Wananchi wa Wilaya ya Maswa leo tarehe 09 Desemba 2024 wameadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya taasisi za umma ambapo kiwilaya maadhimisho hayo yamefanyika katika shule mpya ya sekondari inayojegwa katika Kijiji cha Isageng’he Kata ya Sukuma ambapo zaidi ya miti mia tatu imepandwa na Watumishi pamoja na Wananchi wa kijiji hicho.
Akizungumza na wananchi baada ya zoezi la upandaji wa miti Mkuu wa wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge amewashukuru wananchi wa kijiji cha Isageng’he kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upandaji wa miti lililofanyika katika eneo ambalo shule mpya ya sekondari inajengwa, ambapo serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 584.
Aidha Mkuu wa Wilaya amewapongeza viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri, Watumishi na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuitikia wito wa maelekezo ya serikali ambayo Mhe Rais alitoa maelekezo kwa viongozi kupanda miti, kufanya usafi katika maeneo ya taasisi mbalimbali za serikali.
Mhe Kaminyoge amesema Dkt Samia Suluhu Hassan ni championi wa mabadiliko ya tabia nchi kwa kuendelea kugawa majiko ya nishati safi ambayo itasaidia wananchi kuepukana na matumizi ya kuni na mkaa ili miti inayopandwa iendelee kutunzwa kwa ajili ya vizazi na vizazi.
Pia Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi wa Maswa kurudisha uoto wa asili ambao ulikuwepo enzi za mababu kwa kuwa miti inayopandwa ndio chanzo cha mvua.
“Tukipanda miti kama hivi majumbani, kwenye taasisi tunaongeza uwezekano wa kupunguza mabadiliko ya tabianchi sisi kama wananchi, mmoja mmoja nyumbani, vikundi tunahitaji kupanda miti”
Aidha Mhe Kaminyoge ametoa maagizo kwa viongozi na wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha wanakuwa walinzi wazuri wa eneo lililopandwa miti ili mifugo isiharibu miti iliyopandwa na baada ya miaka mitatu faida ya miti hiyo ipatikane.
Sambamba na hilo pia amewataka wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS ) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha kuwa miti milioni moja na laki mbili iliyobaki igawiwe kwa wananchi pamoja na taasisisi ili lengo la wilaya kufikia miti milioni moja na laki tano likamilike
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Duttu Lubinza amesema kuwa mikakati ya halmashauri ni kupanda miti milioni moja na laki tano ambapo mpaka sasa tayari miti zaidi ya laki tatu imepandwa katika taasisi za umma na watu binafsi.
Aidha ameongeza kuwa ili kufanikisha zoezi hilo Halmashauri kwa kushirikana na wakala wa misitu Tanzania tayari imeweka vitalu katika shule za msingi na sekondari ambavyo vimebeba miche milioni moja na laki tano ili ifikapo januari 2025 miti hiyo ipandwe na ugawaji wa miti unafanyika bure kwa wananchi ili waone umuhimu wa kuhifadhi misitu.
Kwa upande wake Saimoni Japhet amemshukuru Mhe DC Kaminyoge kwa kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru katika kijiji hicho kwa kupanda miti ambapo wameahidi kusimamia kikamilifu ili wananchi wasiingize mifugo yao katika eneo hilo ambalo limepandwa miti na kuwataka wanachi wenzake wakawe mabalozi katika kusimamia eneo hilo.
PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.