Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewataka wanafunzi wa shule ya sekondari Dakama kusoma kwa bidii kwa kuwa serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan imejenga miundombinu bora ya kujifunzia.
Waziri Aweso ametoa ujumbe kwa wanafunzi wa Maswa wenye kauli mbiu isemayo "Acha nisome, Maswa inanitegemea" wenye lengo la kuwahamasisha kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao.
Waziri Aweso amesema hayo wakati akizindua shule mpya ya Dakama yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 584 pamoja na kuongea na wananchi wa Kata ya Dakama Wilayani Maswa tarehe 27 Oktoba 2024.
Pia Waziri ametoa wito kwa wanafunzi kusoma kwa bidii, kuwaheshimu walimu wanaowafundisha pamoja na kusikiliza ushauri, maelekezo na mafunzo yanayotolewa na walimu hao ili waweze kufanikiwa katika Maisha yao.
"Kupitia Elimu mtoto wa mama ntilie anaweza kuwa Daktari bigwa katika Taifa hili, kupitia Elimu mtoto wa mfugaji anaweza kuwa Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka hapa Dakama, naomba msome hakuna kisingizio kwa kuwa sasa Elimu ni Bure kabisa." amesema Waziri Aweso
Aidha Waziri Aweso amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Kamati ya Uinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Chama Cha Mapinduzi kwa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Pia Waziri Aweso ametoa pongezi kwa Mhe mbunge wa Maswa mashariki pamoja na Diwani wa Kata ya Dakama kwa kupambania mradi huo kufika katika Kata hiyo kwa ajili ya kuwahudumia watoto wa Kata hiyo.
Sambamba na hilo Waziri Aweso amesema serikali imetoa kiasi cha shs milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mwalimu katika shule ya sekondari Dakama.
Pia Waziri Aweso ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024 ili kupata viongozi ambao watafanya kazi ya kupeleka maendeleo katika maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.