Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa amewapongeza wakazi wa Maswa kwa kupata mradi wa barabara ya mchepuko (By pass) yenye urefu wa kilometa 11.3 ambapo serikali ya awamu ya sita ilitoa Fedha kiasi cha shilingi bilioni 13.4 kwa ajili ya ujenzi huo lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari kwa wananchi wa Maswa hususani mjini.
Amezungumza hayo leo tarehe 07.10.2023 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua barabara ya mchepuko maarufu by pass ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami katika wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.
Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu kwa kuwajali watanzania ambapo ametoa kibali cha shilingi bilioni 16.2 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi ambao mtandao wa barabara ulipika katika maeneo yao.
Aidha Mhe Bashungwa amempogeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo anaifanya ya kujenga mitandao ya barabara nchi nzima, madaraja ya kimkakati pamoja na miradi mingine inayotekelezwa na wizara hiyo
Pia Waziri wa Ujenzi amepokea ombi la wabunge wa majimbo yote mawili ya Wilaya ya Maswa kuhusu ujenzi wa barabara itakayounganisha Maswa mpaka Malampaka ambapo kituo kikubwa cha reli ya kisasa kinajengwa Malampaka lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi wa maeneo mbalimbali kufika kwa urahisi.
"Kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kipande hiki cha takribani kilometa 10 kinachounganisha mji wa Maswa na reli ya kisasa mpaka Malampaka, sasa sisi wawakilishi wa Rais tuchukue ombi lenu na kulipeleka kwa Rais na kuelezea umuhimu na mkakati mzuri wa kuunganisha mji wa Maswa na kituo kikubwa cha reli ya kisasa ili huduma ya SGR itakapokuwa inapita eneo hilo basi mizigo itakayokuwa inapakuliwa pale na abiria waweze kufika Maswa na kuendelea na safari sehemu nyingine". amesema Mhe Bashungwa
Mhe Bashungwa amewasisitiza wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya kusimamia miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha wote wanaohujumu miundombinu ya barabara hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao na wizara itashirikiana nao kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa.
Pia ametoa wito kwa wakandarasi wote wakiwepo wazawa kuwa serikali itahakikisha inafanya kazi na wakandarasi wote ambao watafanya kazi kwa weredi kwa mujibu wa mkataba ambao wamekubaliana na serikali kupitia wizara ya ujenzi.
Nae Meneja wa Tanroad Mkoa wa Simiyu Mhandisi John Mkumbo amesema barabara hiyo iko katika hatua za mwisho ambapo mpaka sasa imekamilika kwa asilimia 99 na vitu vichache vimebaki ili ikamilike ikiwepo uwekaji wa alama barabarani pamoja na vibao vya pembeni.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.