Wanawake na vijana wajasiriamali wilayani Maswa Mkoani Simiyu wamepata mafunzo ya elimu ya fedha pamoja na uundwaji na usajili wa vikundi ili kuwawezesha kupata mikopo isiyo na riba.
Hayo yamezungumzwa na Afisa mahusiano benki ya CRDB tawi la Maswa Ndugu Matensa Lugumba wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa yaliyohusisha wanawake na vijana wajasiriamali wa wilaya ya maswa.
Ndugu Lugumba amesema kuwa lengo la benki hiyo ni kuinua uchumi wa wananchi waliopo Maswa na Taifa kwa ujumla kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine ili kuondokana na mikopo ya kausha damu kwa kuwa mkombozi amepatikana ambaye ni CRDB benki.
Ameongeza kuwa benki ya CRDB kupitia huduma ya CRDB foundation wamekuja na huduma ya iMBEJU ambapo huduma hiyo ni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vijana na wanawake kupitia kwenye vikundi ambapo mikopo hiyo itaanzia shilingi 200,000 mpaka shilingi milioni 5,000,000 na itatolewa bila riba.
Lengo la mikopo hiyo ni kuwainua vijana na wanawake kibiashara ambapo ili mjasiriamali apate mkopo huo ni lazima awe amesajiliwa katika kikundi ambapo benki itaingia mkataba na kikundi kwa ajili ya kumdhamini mjasiliamali atakayehitaji mkopo.
Pia amesema kikundi lazima kiwe na akaunti ya CRDB ambapo kikundi hicho kinatakiwa kiwe na wanachama hai ambao ni waadilifu, wanaofahamiana na wenye malengo thabiti ambayo yataweza kuzaa na kuleta faida.
Ameongeza kuwa mwanakikundi anaweza kupata mkopo moja kwa moja CRDB ilimradi wadhamini wake ni kikundi ampabo viongozi wao watakuwa wamemsainia na awe anajishughulisha na shughuli yoyote ya ujasiriamali.
Kwa upande wake Afisa vijana kutoka Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Ndugu Berther Lugenji amesema sifa za mjasiriamali anatakiwa kuwa mbunifu mwenye nidhamu ya fedha, mwenye kusimamia mawazo aliyonayo, kujua namna ya kutafuta masoko na kutumia changamoto kuwa fursa katika ujasiriamali anaoufanya ili kufikia malengo.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Rodgers Lyimo amewataka wafabiashara ndogondogo kufika katika Ofisi ya Maendeleo ya jamii kwa ajili ya kujisajiri ili waweze kupata vitamburisho vya ujasiriamali ambavyo vitadumu kwa miaka mitatu.
Pia amewashukuru benki ya CRDB kwa kutoa elimu hiyo ambayo itawasaidia vijana na wanawake wajasiriamali kupata mikopo katika benki hiyo sambamba na hilo amewasisitiza wajasiriamali hao kuchangamkia fursa hiyo kwa kuunda vikundi na kufungua akaunti ili wapate mikopo hiyo isiyokuwa na riba.
Lucy Misinzo ambaye ni afisa maendeleo ya jamii amesema kuna aina mbili ya usajili wa vikundi ambapo kuna usajili wa vikundi vya kijamii na kifedha ambapo ili vikundi vya kijamii visajiliwe kikundi kinatakiwa kiwe na muhtasari wa kuonyesha kikundi kimeadhimia kusajiliwa, katiba pamoja na barua ya maombi iliyopitishwa na Mtendaji wa Kata.
Aidha ameongeza kuwa ili kikundi cha kifedha kisajiliwe kinahitaji muhtasari, katiba, barua ya maombi na fomu ya azimio la kusajili kikundi cha kifedha pamoja na mtu atakayekuwa anatoa elimu kuhusu masuala ya fedha.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.