Afisa mbogamboga na matunda kutoka Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Masalu Shibiliti Lusana ametoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya lishe bora ili kuepukana na magonjwa.
Akizungumza na wananchi katika mkutano huo uliofanyika tarehe 14 February 2023 katika viwanja vya mnadani vilivyopo Kitongoji cha Mnadani Kata ya Nyalikungu Ndg. Shibiliti amewaeleza wananchi umuhimu wa matumizi ya mbogamboga, matunda, viazi lishe na mahindi lishe jinsi ambavyo inasaidia kinga ya mwili, kuongeza uono na kutokuzeeka mapema kwa kuwa vyakula hivyo vina viini lishe na virutubisho ambavyo havipatikani sehemu nyingine.
Pia Afisa mbogambonga amewaomba wanachi kulima mbogamboga mfano mchicha, kunde, chainizi na matunda ya asili kama vile limbe, machungwa, mapapai na ukwaju ambapo mwananchi mwenyewe anaweza kulima nyumbani kwake kwa kuwa itamsaidia kuepukana na matumizi ya mboga ambazo zimelimwa na kupuliziwa viuatilifu ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa.
Ndg. Shibiliti amewasisitiza wananchi kulima malando lishe kwa kuwa ni lando linalokomaa haraka, Lina mavuno mengi ya viazi vya njano ambavyo vina virutubisho vingi pamoja na mahindi lishe ambayo yana kiini tete Cha njano ambacho ni muhimu kwa wazee kujenga kinga ya mwili.
Nae Afisa udongo kutoka Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Charles Maganga amewahakikishia wananchi hao udongo wa maeneo yao ni mzuri kwa kilimo Cha mbogamboga, matunda pamoja na viazi lishe hivyo wananchi hao wanatakiwa kulima maana tafiti zilishafanyika na kuonyesha matokeo mazuri hasa katika viazi lishe ambavyo vimefanya vizuri katika Kata ya Shishiyu.
Kwa upande wake mtaalamu wa Mifugo Kata ya Nyalikungu Ana amewashauri wananchi kutumia nyama nyeupe ambazo ni kuku, samaki na dagaa kwa kuwa ina virutubisho vizuri ambavyo vitasaidia kuukinga mwili na magonjwa mbalimbali kama vile kansa na magonjwa mengine.
Nae mwenyekiti wa kitongoji cha mnadani amewashukuru wataalamu wa lishe kwa kuwapatia elimu hiyo na wameahidi kuitekeleza kwa vitendo kwa kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao kwa kuandaa mashamba darasa ili wananchi wapate elimu hiyo kwa vitendo na kuepukana na ulaji mbovu wa vyakula usiofata lishe Bora.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.