Maafisa kutoka Divisheni ya Elimu Sekondari Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wamefanya ziara katika shule za Nguliguli Sekondari na Senani Sekondari kuzungumza na Walimu masuala ya taaluma, nidhamu, kutatua changamoto katika mazingira ya kazi na kutambua wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalumu.
Akizungumza na walimu hao katika shule hizo Afisa Elimu Taaluma kutoka Divisheni ya Elimu Sekondari Wilaya ya Maswa Ndg. Khalfan Millongo amewaomba walimu kusimamia nidhamu katika shule na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuongeza ufaulu katika shule zao ziweze kushika nafasi za juu kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha Pili na Cha Nne.
Afisa Elimu Taaluma wilaya amewapongeza walimu wa Biolojia katika shule ya Sekondari Nguliguli kwa kufaulisha wanafunzi kwa wastani wa C ambayo ni GPA ya 3.35 na walimu wa Kiswahili na Kemia katika shule ya sekondari Senani waliyofaulisha masomo hayo kwa wastani wa GPA ya 3. Kiswahili na Kemia 3.3
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Elimu Maalumu kutoka Divisheni ya Elimu Sekondari wilaya Mwl. Kassongo amewaomba walimu kutoa takwimu za wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalumu katika shule hizo ili serikali iweze kuwatambua na kuwawezesha vifaa vya kuwasaidia katika kusikia kutembea na kuona.
Aidha Kassongo amewasisitiza walimu kuwa serikali imeweka mambo muhimu na msingi yasimamiwe ambapo Maafisa wa Elimu Wilaya, Maafisa Elimu Mkoa , Maafisa Elimu Kanda pamoja na Walimu Wakuu wameagizwa kuwa taasisi zote wapande miti ambapo kwa wastani mwanafunzi anatakiwa kuwa na miti kuanzia 3 anayoitunza na wanatakiwa kusimamia kikamilifu.
Serikali imesisitiza kila Shule wahakikishe wanasimamia huduma ya utoaji wa chakula ambapo Kamati za Shule na Bodi wapewe elimu ili washirikiane na walimu kwa kuwa wabunifu kwa kulima mashamba ambayo yatawasaidia kuzalisha chakula ili kutekeleza majukumu ya serikali na wanafunzi waweze kusoma vizuri ili kuongeza ufaulu kwa sababu wanafunzi watapata chakula eneo la shule.
Kwa upande wao walimu wameomba serikali kuwajengea nyumba maeneo ya Shule ili kurahisisha ufundishaji kwa sababu wanapoishi sasa ni mbali na Shule hivyo kupunguza ufanisi katika kazi yao ya kufundisha na kusababisha ufaulu wa wanafunzi kutokuwa mzuri.
Vilevile upungufu wa walimu wa kike katika baadhi ya shule imekuwa changamoto kwani wanafunzi wa kike wanashindwa kueleza shida zao ambazo walimu wa kike walitakiwa kuzisikiliza pamoja na kuzitatuana ambapo shule 6 za sekondari Wilaya ya Maswa hazina walimu wa kike ikiwepo Nguliguli Sekondari.
Wakijibu changamoto hizo Maafisa Elimu hao wameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo zilizotolewa na walimu na kuwaomba walimu kufanya kazi kwa ushirikiano kuanzia darasani mpaka nje ya darasa ili kuongeza ufaulu na kufuata Sheria na miongozo yote iliyotolewa na serikali katika kutimiza majukumu yao na kusisitiza muda wa michezo uzingatiwe katika shule hizo .
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.