Shirika la Nutrition International kwa ushirikiano na World Vision - Tanzania chini ya uangalizi wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wamefanya uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wa kutathmini hali ya jinsia, vijana balehe na lishe katika mkoa wa Simiyu. Utafiti huu ni sehemu ya mradi uitwao “Realizing Gender Equality, Attitudinal Change, Transformative Systems in Nutrition-(REACTS-IN)” unaotekelezwa katika wilaya za Maswa na Meatu, Mkoa wa Simiyu. Utafiti huu ulifanyika ili kupata taarifa zitakazotumika kuandaa utaratibu wa kupangilia mradi wa REACTS IN na kuhakikisha kuwa mradi huu unafikia malengo yake ya kuwainua vijana rika balehe walio katika mazingira magumu, ili kukidhi mahitaji yao muhimu ya usawa wa kijinsia na lishe. Uwasilishaji wa matokeo haya ya utafiti ulilenga kuwajulisha wadau wote muhimu wa mradi hali halisi ilivyo kuhusiana na hali ya usawa wa kijinsia na lishe miongoni mwa vijana balehe katika mkoa wa Simiyu ili kubaini na kupanga mikakati halisia itakayoweza kuboresha huduma za afya ya uzazi na lishe kwa vijana balehe.
Matokeo ya utafiti huo yameonyesha kwamba, vijana balehe wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma stahiki za lishe na afya ya uzazi na jinsia kutokana na mila na desturi, ndoa za mapema kwa wasichana na changamoto za mifumo ya kutolea huduma katika jamii. Hali kadhalika, ingawa Serikali imeweka mikakati mizuri na yenye tija kuwahudumia vijana balehe wa makundi yote, jamii kwa ujumla wake bado haijajipanga kiasi cha kutosha kuwahudumia vijana balehe wenye mahitaji maalumu katika maeneo mbalimbali kama vile mashuleni, katika vituo vya kutolea huduma za afya n.k.
Ushauri umetolewa kwa Serikali ya Mkoa na wadau wake kuishirikisha jamii katika kukuza uelewa wa masuala ya haki ya kijinsia, lishe na afya ya uzazi kwa vijana balehe ili kusaidia ukuaji wenye tija wa kundi hili maalumu la vijana kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.