Walimu wa awali kutoka shule 135 za msingi Wilayani Maswa wamepatiwa mafunzo maalumu ya mbinu bora za kufundisha wanafunzi wa madarasa ya awali ili waweze kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na kumudu madarasa makubwa. Mafunzo hayo yametolewa na progammu ya Shule Bora katika ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana Maswa iliyopo Kata ya Sukuma Wilayani Maswa Mkoani Simiyu.
Afisa Elimu Taaluma ambaye pia ni Mratibu wa Shule Bora Wilaya ya Maswa Mwl. Neema Makundi alisema mafunzo waliyoyapata walimu hao yatawaongezea uwezo wa kumudu madarasa kutengeneza zana mbalimbali ambazo zitawavutia wanafunzi na kuongeza maudhurio na kuwafanya watoto hao kusoma kwa urahisi.
Pia Mwl Makundi alitoa wito kwa walimu hao baada ya kupata mafunzo hayo wakalete mabadiliko katika shule zao kwa kupunguza idadi ya watoto wasiojua KKK na kuongeza maudhurio pamoja na upendo kwa watoto katika madarasa yao.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Ualimu Bunda Mwl. John Ndimbo alisema mbinu walizozipata walimu zitaenda kusaidia watoto kumudu stadi za KKK na kumudu madarasa makubwa.
“Katika mafunzo haya watoto wamewezeshwa mbinu na moja ya mbinu hizo ni nyimbo, michezo na ngojera ambazo walimu wanaweza kuzitumia ili kulifanya darasa kuwa changamfu pamoja na kuwafikia watoto wote kulingana na mahitaji yao.” Alieleza Mwl. Ndimbo
Aidha aliwasisitiza kuwa serikali imetumia gharama kuandaa mafunzo hayo hivyo amewataka walimu hao mafunzo waliyoyapata waende wakayatekeleze kwa weredi ili kuweza kupunguza changamoto za watoto kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kwa upande wake Mwalimu wa shule ya msingi Inenwa Mwl. Paul Julius alisema baada ya mafunzo hayo ufundishaji utarahisishwa kwa kuwa wamepata mbinu bora za kutengeneza dhana na kumudu ufundishaji wa madarasa makubwa ya wanafunzi.
Nae Mwl. Lilian Israel kutoka shule ya msingi Mwasayi alisema mafunzo hayo yamewasaidia kuboresha namna ya kufundisha watoto kwa kutumia mbinu na dhana za kufundishia ambazo watoto wakiziona watafurahia na kuelewa kwa haraka kwa kuwa zitakuwa zinajieleza zenyewe.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.