Walimu Wakuu, Maafisa Elimu Kata na Wenyeviti wa Kamati za shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wameanza mafunzo ya siku tatu yenye lengo la kushirikisha wazazi katika kuboresha utoaji wa elimu bora jumuishi na salama kwa watoto wote.
Mafunzo hayo yameandaliwa na mradi wa shule bora unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UK Aid kwa lengo la kuwajegea uwezo washiriki kwa ajili ya kuimarisha shughuli za UWaWa.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo ya UWaWa yaliyoanza Leo tarehe 6 march 2023 Katibu Msaidizi wa TSC Masenyi Kisika amesema mafunzo hayo yatahusisha wazazi kwa sababu mwalimu wa kwanza wa mtoto ni mzazi wake nyumbani hivyo amewataka walimu wakuu, maafisa elimu kata na wazazi kushirikiana ili kuhakikisha watoto hao wanakuwa katika hali nzuri ya kitaaluma.
Pia ameongeza kuwa wenyeviti wa kamati za shule ndio wawakilishi wa wazazi shuleni hivyo elimu watakayoipata katika mafunzo hayo wakaieneze vema kwa wazazi wengine ili kuhakikisha watoto wanapata mahitaji ya muhimu.
Aidha, amesisitiza kuwa mwalimu mkuu ndio meneja wa shule kwa hiyo ni wajibu wake kuhakikisha kuwa mambo yote yanaenda vizuri katika shule yake, pia Afisa Elimu Kata ndio msimamizi mkuu wa taaluma katika Kata, msimamizi wa wazazi kwa hiyo ushirikiano baina ya wazazi utakuwa mzuri na utazalisha mazao mazuri kwa watoto.
“Ni mategemeo yangu kwamba baada ya mafunzo haya kutakuwa na mabadiliko sana katika shule zetu kwa sababu wote mnaohusika yaani figure zote zinazoshughulika na suala la mtoto mzazi, mwalimu mratibu elimu kata wote mko hapa. Baada ya hapa tunategemea kuwa na zao zuri, tunategemea kunyanyuka kitaaluma, tunataka tupate watoto ambao baadae watalisaidia taifa letu” Amesema Kisika
Awali akitoa taarifa Afisa elimu taaluma msingi wa Wilaya ya Maswa ambaye pia ni mratibu wa mradi Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Neema Makundi amesema mafunzo hayo yatafanyika siku tatu kwa Kata zote kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza imehusiha Kata 12 ambazo ni Ipililo, Jija, Mataba, Budekwa, Mwabaraturu, Senani, Dakama, Isanga, Sangamwalugesha, Masela, Mpindo na Shishiyu.
Mafunzo hayo yameanza kwa wakufunzi kutoa mazoezi katika makundi kuona matokeo ya darasa la saba na la nne yalivyokuwa katika shule zao kwa kila Kata ili kuona mbinu, changamoto na namna ambavyo wazazi wameshiriki katika kusaidia ufaulu wa watoto wao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.