Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Nchini imewawezesha Walimu wapatao (50) kutoka shule za msingi 50 kupata mafunzo ya ufundishaji na ujifunzaji jumuishi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku 4 ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kupitia program ya Shule Bora yamefadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UKAID.
Ester Marwa Mratibu wa Elimu bora ngazi ya Mkoa alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia.
Marwa aliongeza kusema kuwa mafunzo hayo yanawajengea uwezo Walimu kuweza kuwatambua watoto wenye mahitaji maalumu na kujua mbinu rafiki na jumuishi za kujifunzia.
“Mkoa kwa sasa una zaidi ya wanafunzi (605) wenye mahitaji maalumu na mwaka huu 2023 pekee tumeandikisha wanafunzi 234, hivyo unaweza ukaona ambavyo elimu bora ilivyochangia kuongeza usajili wa wanafunzi”Alisema Marwa.
Mwl Neema Makundi Afisa Elimu taaluma Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na Mratibu wa Elimu bora Wilayani Maswa alisema kuwa anaishukuru Serikali kwa kuwaletea mafunzo hayo kwa kuwa yatasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuweza kujifunza.
“Mafunzo haya yanawasaidia walimu kujua mbinu za kujifunza maana wamefundishwa mbinu za kufundishia na namna ya kutengeneza zana za asili za kujifunzia ili watoto wote waweze kupata fursa ya kujifunza”.Alisema Makundi.
Mwl Salimu Kidunda kutoka Shule ya Msingi Nyasosi Kata ya Ngulyati Wilayani Bariadi Mkoani hapa alisema kuwa mafunzo hayo yamesaidia kuandaa dhana za kufundishia na kuwatambua watu wenye mahitaji maalumu.
“Mafunzo haya yamenisaidia kujua makundi ya watu wenye ulemavu na kujua alama za kufundishia kwenye elimu jumuishi na kuweza kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu kuweza kuzifikia ndoto zao.”Alisema Kidunda.
Mwalimu Ferister Mkenda toka Shule ya Msingi Budalabujiga “A” alisema kuwa mafunzo haya yametusaidia walimu kwenda kuwasaidia wazazi walio na watoto wenye mahitaji maalumu.
“Kama walimu tumefundishwa kwenda kuwa daraja kati ya wazazi na kuwapa elimu juu ya umuhimu wa elimu ili wazazi waone umuhimu wa kusomesha watoto wenye mahitaji maalumu”.Alisema Mkenda.
Nae Kisandu Mkazi wa Biafra Wilayani hapa alisema kuwa anaishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya watoto wenye mahitaji maalumu kuweza kujifunza, huku akitoa rai kwa Serikali kuweza kuongeza walimu.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ila tunaiomba Serikali iongeze walimu, kwa mfano Shule ya msingi Binza inamwalimu mmoja anaefundisha watoto wenye mahitaji maalumu kuna wakati watoto wetu hawapati masomo inapotokea Mwalimu anaudhuru.” Alisema Mzazi huyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.