Balozi wa Pamba Tanzania Mhe. Agrrey Mwanri amesema Serikali imepanga kuleta mbegu na viuatilifu bure kwa wakulima wa pamba lengo likiwa ni kupunguza makali ya soko ambalo limewaathiri kwa mwaka huu pamoja na kutoa elimu ya namna bora ya kulima kwa kufuata kanuni za kilimo cha pamba ikiwepo kuandaa shamba mapema baada ya msimu wa mavuno kukamilika.
Balozi wa pamba nchini Tanzania Mhe. Agrrey Mwanri amewataka wakulima wa pamba kuzalisha kwa wingi zao hilo kwa ubora unaotakiwa ili liwe na tija katika soko la Dunia ambapo katika msimu huu zao hilo limelimwa kwa wingi na nchi nyingi Duniani hivyo kusababisha mdololo wa bei katika soko.
Aidha balozi wa pamba alisema msimu uliopita bei ya pamba ilikuwa juu kutokana na wazalishaji wengine huko Duniani hawakulima pamba kutokana na COVID-19 hivyo kufanya bei iwe juu tofauti na sasa ambapo nchi zote ambazo hazikuzalisha zao hili kipindi hicho zimezalisha msimu huu na kusababisha pamba kuwa nyingi.
Mhe. Mwanri amesema hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa katika ziara yake katika Kijiji Cha Buyubi na Dodoma katika Kata ya Mwamashimba wakati akiwa katika mkutano wa Kijiji kwa lengo la kuwaelimisha wakulima wa pamba namna bora ya kuvuna pamba nzuri ambazo zitaweza kupata soko kimataifa kutokana na ubora wake.
“Tukizalisha pamba nyingi hapa na bei ikaanguka kule duniani bado hela yetu itakuwa nyingi kwa sababu itakuwa na ubora na wingi unaotakiwa kulinganisha na bei iliyopo” amesema balozi wa pamba.
Pia amewataka wakulima kushirikiana kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake kwa kuelimishana wao kwa wao jinsi ya kulima pamba ili kujipatia fedha nyingi.
Nae Diwani wa Kata ya Mwamashimba Mhe. Saida Daudi Dila amewataka wananchi kuzingatia elimu waliyopewa na Balozi wa pamba kwa lengo la kumkomboa mkulima kiuchumi kwa kupata elimu ya kanuni bora za kilimo cha pamba.
Pia Mheshimiwa Diwani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pampu za kupulizia wadudu pamoja na viutalifu bure, hivyo amewaomba wananchi kutumia fursa hizo ambazo Rais amewapa ili ziwasaidie katika shughuli zao.
Aidha amewasisitiza wananchi wake kuvuna pamba kwa kufuata kanuni ili kuepuka pamba chafu ambazo hazistahili katika soko hivyo kusababisha kipato chao kushuka na kukosa wanunuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Maisha Mtipa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawezesha wakulima wa pamba kwa hali na mali kwa kutoa pembejeo na mbolea ambazo zitawasaidia kujipatia kipato watakapovuna pamba yao.
Mkuu wa Wilaya ameishukuru Serikali pamoja na Mkurugenzi wa bodi ya Pamba Tanzania kwa kumleta Balozi wa Pamba katika Wilaya ya Maswa kwa kutoa elimu ambayo imekuwa chachu kwa wakulima wa pamba kuanza kutumia kanuni bora za kilimo cha pamba na kuzalisha kwa tija.
Pia Mhe. Kaminyoge amewataka watendaji wote kuanzia ngazi ya Halmashauri kusimamia kwa karibu wakulima wa pamba kwa kutoa Elimu kuhusu kanuni bora na Sheria ili kuzalisha kwa tija zao hilo.
Halmashauri inatarajia kulima Jumla ya Hekta 82,212.4 za zao la pamba katika msimu wa Kilimo wa 2022/2023 na kutarajia kupata mavuno ya Tani 102,765.06, mpaka kufikia mwishoni mwa msimu wa Kilimo Cha pamba jumla ya Hekta 87,438.06 za zao la pamba zimelimwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambapo ni sawa na asilimia 106.35.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.