Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amewataka wadau wote wa maafa kutoa Elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari kuhusu maafa lengo likiwa ni kuwajengea uelewa wananchi namna ya kujilinda pindi mvua hizo zitakapoanza.
Pia mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuimalisha nyumba zao na kuchukua tahadhari na hatua madhubuti kwa kuhakikisha watoto wao wanakuwa karibu na makazi yao pindi watakapoona dalili za mvua kuanza.
Ameongeza kuwa katika msimu huu mvua za vuli zitanyesha kuanzia mwezi Oktoba hivyo Mamlaka ya hali ya hewa imetoa utabili kuwa mvua zitanyesha juu ya wastani ambapo zitasababisha madhara kwa watu na miundombinu.
Mkuu wa Wilaya amesema hayo katika kikao kazi cha kamati ya maafa kilichowashilikisha wadau mbalimbali kutoka taasisi mbalimbali za kidini, mashirika yasiyo ya kiserikali taasisi za kiserikali, wataalamu pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
"Kama watendaji wa umma tuna kila sababu ya kuchukua maelekezo ya Rais na kuwatahadhalisha wananchi juu ya jambo hilo, na kama maafa yakiwakuta tuna kila sababu ya kuchukua hatua kuhakikisha tunawanusuru uhai na Mali zao, tuna kila sababu ya kunusuru miundombinu mbalimbali itakayoathirika na jambo hilo, miundombinu ya barabara, afya, Elimu, na maji." Amesema Mkuu wa Wilaya
Pia mkuu wa Wilaya amewataka viongozi wawe wepesi wa kutoa taarifa linapotokea tatizo kwa kushiriki pamoja kunusuru sehemu ambazo maafa hayo yametokea kuliko kusubiri viongozi wa juu kwenda kutatua changamoto hiyo.
Aidha Mhe Kaminyoge ametoa wito kwa Mamlaka mbalimbali ikiwepo wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA), wananchi waliopo mjini, pamoja na Mamlaka zingine zote kuhakikisha wanasafisha mifereji yote iliyopo mjini mpaka eneo ambalo maji hayo yanaenda katika mito ili kuepusha wananchi kupata mafuriko.
"Endapo maafa yametokea mahali, hatua ya kwanza ni kutoa taarifa kwa ngazi zote kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu kwa kuchukua hatua kwa kadri ya uwezo walionao kama ni serikali ya Kijiji basi wananchi waungane na viongozi kuweza kuwasaidia wananchi waliopata maafa hayo wakati serikali inajulishwa." Mhe. Kaminyoge amesema
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Vivian Christian ametoa mwezi mmoja kwa watendaji wa Kata wawaelimishe viongozi wengine sambamba na wananchi kuhusu namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya maafa ili wananchi wawe na uelewa huo.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe. Paul Maige amesema jukumu kubwa la viongozi ni kuhakikisha wananchi wanakuwa salama endapo maafa yatatokea kwa kuwa watendaji wanayajua maeneo yao vizuri ambayo yalikuwa yanatumika kwa Kilimo na sasa ni makazi endapo kutatokea maafa ofisi ya Mkurugenzi ipate taarifa mapema ili iweze kuchukua tahadhari mapema.
Katika kikao hicho kamati ya maafa ilitoa mada mbalimbali kuhusu masuala ya maafa ambazo zitawasaidia washiriki kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ambazo zitanyesha juu ya wastani.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.