Vitendo vya ukatili katika Wilaya ya Maswa vimepungua kutoka 671 mwaka 2023 hadi kufikia 591 kwa mujibu wa rekodi za kuanzia mwezi januari hadi mwezi Desemba mwaka huu.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa Ndg Athuman Kalaghe akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Maswa alisema kuwa maadhimisho hayo ni kuikumbusha jamii kupinga ukatili unaoendelea katika jamii zao ambapo serikali imetunga sera, sheria na miongozo mbalimbali itakayosaidia kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Pia Ndg, Kalaghe alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa haraka za ukatili kwa wataalamu waliopo katika maeneo yao ili wale waliofanyiwa vitendo hivyo wapate msaada.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema “Kuelekea Miaka 30 ya Beijing chagua kutokomeza ukatili wa kijinsia”
Aliongeza kuwa kauli mbiu hiyo inasisitiza mtu binafsi na jamii kwa ujumla kuchukua hatua madhubuti za kupinga, kukataa na kukemea ukatili wa kijinsia na kutoa nafasi kwa kila mtu kufanya tathmini kuelekea miaka 30 ya kupinga ukatili.
Pia Katibu Tawala alieleza kuwa takwimu zinaonyesha vitendo vya ukatili vinatokea zaidi kwa wanawake na watoto ikiwa ni kundi linalopitia changamoto nyingi za ukatili kutokana na mgawanyiko usio sawa wa majukumu katika familia hivyo ni muhimu sana kuimarisha maendeleo na ustawi wa watoto ili kupunguza changamoto zinazowakabili.
Katibu Tawala alieongeza kuwa uwepo wa vitendo vya ukatili unapelekea kuwa na ulemavu wa kudumu, mimba za utotoni, magonjwa mbalimbali ya kuambukiza, vifo, matatizo ya kisaikolojia, kujiua, umaskini uliokithiri pamoja na kupoteza nguvu kazi.
Aidha alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutokomeza ukatili wa kijinsia ikiwemo kampeni maalumu 16 za kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Akitoa taarifa Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Maswa Bi. Lilian Clement alisema kuwa sababu za kupungua kwa vitendo hivyo vya ukatili ni kutokana na Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwepo Shirika la World Vision, Ustawi wa Jamii, Divisheni ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Radio SIBUKA kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wananchi.
Maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yalifanyika Kiwilaya katika Kata ya Senani ambapo kata nne zilihudhulia maaadhimisho hayo ikiwepo Ngulinguli, Mpindo, pamoja na Mwamanenge tarehe 10 Desemba, 2024.
Ameeleza kuwa Katika maadhimisho hayo kazi zilizofanyika katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilikuwa ni kutoa elimu Redio SIBUKA, kutoa elimu katika Hospitali ya Wilaya kutoa elimu kupitia mikutano ya hadhara kwa Kata za Shishiyu, Kadoto na Jija, kutoa elimu mashuleni pamoja na maeneo mengine.
Pia aliongeza kuwa takwimu za ukatili zimepungua kutokana na matokeo chanya ya harakati za mapambano hayo kutoka kwenye mamlaka na wadau.
Kwa upande wake meneja mradi wa REACT-IN Dr. Stanford Kaserwa alisema shirika la world vision kupitia mradi wa REACT-IN kwa kushirikiana na serikali wameendelea kupambana na vizuizi hivyo kwa kuiwezesha jamii kubadili mitazamo katika masuala ya usawa wa kijinsia na masuala ya ukatili kwa ujumla katika sekta ya afya na lishe.
Pia alibainisha kuwa World Vision inashirikisha wanaume na vijana wa kiume wawe chachu katika jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.