Viongozi walioshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024 wameapishwa leo tarehe 29 Novemba 2024 kwa lengo la kuanza utekelezaji wa majukumu ya kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.
Awali akizungumza na viongozi hao wakati akimwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Maisha Mtipa, Afisa Manunuzi Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bi. Elinight Mmari amesema afisa Uchaguzi ametoa pongezi kwa viongozi wote wa Serikali za Mitaa kwa kuchaguliwa na amewaomba wafanye kazi kwa kufuata misingi, kanuni, taratibu na Sheria.
"Leo tunayo kazi moja tu kabla ya kuanza majukumu yetu tunapaswa kuapa na baada ya kiapo mnapaswa kuanza kazi kwa sababu tayari utakuwa mtumishi halali ambaye umekula kiapo cha kutumikia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wananchi wake." ameeleza Bi. Mmari
Akiwaapisha viongozi hao Hakimu Mkazi Mwandamizi Wilaya ya Maswa Mhe. Enos Misana amewataka viongozi hao kuwa waadilifu na kutunza siri katika majukumu yao kwa kuwa wananchi wamewaamini hivyo jukumu lao ni kuhakikisha hawakiuki viapo hivyo walivyoapa.
Pia Mhe. Misana amewasisitiza viongozi hao kuwa waadilifu na kuwa watii kwa mamlaka zilizo juu yao.
Zoezi hilo limefanyika Wilayani Maswa katika vituo mbalimbali vilivyopangwa kwa ajili ya kuapishwa kwa Viongozi hao ambao ni Wenyeviti wa Vitongoji 510, Wenyeviti wa Vijiji 120 na wajumbe wa Halmashauri za Vijiji.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.