Wananchi wa kijiji cha Mwandete Kata ya Sangamwalugesha wamehamasika kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji chao kwa kuchanga michango ya fedha kwa kila Kaya na kusomba mali ghafi nyingine ili kukamilisha ujenzi huo. Wananchi wa kijiji hiki awamu ya kwanza ya mchango kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati hii ulikuwa shilingi 8,000,000/= ambao waliutumia kuanzisha ujenzi, kwa kushirikiana na Halmashauri, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki na wadau wengine waliweza kujenga hadi hatua ya upauwaji.
Juma lililopita walianzisha mchango awamu ya pili ambao wamekusanya shilingi 6,000,000/= ambazo wameamua kuziwekeza katika ukamilishaji wa jengo hilo.
Kwa kuunga juhudi za Wananchi wa kijiji hiki Mhe. Mbunge ametoa mifuko 50 ya Saruji iliyokabidhiwa na Katibu wake siku ya leo katika eneo la ujenzi.Mkuu wa Wilaya naye ameahidi kuchangia milango yote.
Ujenzi wa jengo hili ulianza tarehe 30/7/2018 na wameahidi kukamilisha tarehe 10/5/2019.
Kutokana na juhudi zilizoonyeshwa na Wananchi hao Mhe. Mkuu wa Wilaya Dr. Seif Shekarage ameahidi kutoa vyeti vya pongezi kwa timu zote mbili zilizofanikisha kukusanya michango hiyo pamoja na uongozi wa kijiji.
Mhe. Mkuu wa Wilaya akiongea na wananchi waliokuwa katika eneo la ujenzi amewasisistiza kuendelea kuwa wamoja ili wawe mfano wa kuigwa Wilayani hapa kutokana na juhudi zao. Pia amewaasa kwa kuwa kipindi hiki ni cha mavuno, watunze chakula walichopata maana hali hewa siyo nzuri. Sambamba na hayo amewashauri kukata Bima ya Afya ya jamii (CHF) ili kuwasaidia kupata huduma ya afya muda wote hata katika kipindi ambacho hawana fedha. Ameongelea suala la kusomesha watoto wao na kuwaonya kuhusiana na suala la kuwapa watoto wa shule mimba.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.