Timu ya Hamasa na Uhamasishaji ikiongozwa na Msanii Mahiri ambaye pia ni Balozi wa Taasisi ya Mtu ni Afya ambayo ipo chini ya Wizara ya Afya Ndg. Mrisho Mpoto imefanya ziara ya siku mbili Wilayani Maswa yenye lengo la kuhamasisha na kutoa elimu ya mtu ni afya kwa wananchi wa wilaya ya Maswa hususani elimu ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Lengo la kampeni ya mtu ni afya ni kuelimisha wananchi kuhusu magonjwa na hatari za kiafya kwa malengo ya kuzuia na kuhimiza wananchi kudhibiti afya zao.
Balozi huyo amezungumza na wananchi wa Kata za Sangamwalugesha, Shanwa na Malampaka kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara ambapo ametoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupingu kwa kuzingatia ujenzi na matumizi bora ya vyoo majumbani, makanisani maeneo ya mikusanyiko pamoja na misikitini.
Pia unawaji wa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwa kuzingatia hatua tano za unawaji nyakati zote mtu anapotoka chooni.
Balozi, Mpoto amegawa masinki ya vyoo, ndoo za maji na matisheti kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kutumia vyoo bora ambavyo vitasaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.
Kwa upande wake Musa Maduhu mkazi wa kijiji cha Sangamwalugesha ameuomba uongozi ngazi ya afya kuwafuatilia kwa ukaribu watu wote ambao hawana vyoo ili wachimbe na kutengeneza vyoo bora ili kuondokana na kipindupindu.
Nae Tadeus Shija Mchungaji wa kanisa la EAGT Sangamwalugesha ameishukuru timu ya hamasa ikiongozwa na balozi mpoto kwa elimu waliyoitoa na amewashauri wananchi wenzake kuacha kuogelea kwenye mabwawa na mito kwa kuwa maji hayo hayana usalama kwa kuwa yanatoka sehemu mbalimbali na kusababisha mtu huyo anayeogelea kupata kipindupindu.
Godfrey masanja mkazi wa Sangamwalugesha ameishukuru serikali kwa kutenga muda kwa ajili ya kutoa elimu na pia akatoa maoni yake ili kipindupindu kiweze kuisha ni lazima kuwe na mpangokazi wa kutembelea nyumba kwa nyumba kutoa elimu kupitia kamati ya ustawi wa jamii.
Regina Masanja mkazi wa Malampaka amewataka wananchi wa Malampaka kuhamasishana wao kwa wao na pia uongozi wa kijiji kuunda kamati ya afya kuwatembelea wananchi hao 36 ambao hawana vyoo ili waweze kujenga vyoo.
Amina Hamisi mkazi wa Malampaka ametoa wito kwa wananchi wenzake wakawe mabalozi wa kujenga vyoo bora katika kaya zao ili kuweza kutokomeza kipindupindu katika Kata ya Malampaka.
Takwimu zinaonyesha katika Kata ya Sangamwalugesha ina zaidi ya kaya 1,624 ambapo kaya zenye vyoo bora 643, kaya zenye vyoo vya shimo 945 na kaya ambazo hazina vyoo ni 36, katika Kata ya Malampaka ina jumla ya kaya 2,779 kaya zenye vyoo bora ni 1,583 kaya zenye vyoo vya asili ni 1,159 na kaya ambazo hazina vyoo ni 37.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.