Kampeni ya uhamasishaji wa elimu bora ya kilimo cha pamba umefanyika katika Wilaya ya Maswa lengo likiwa ni kuwaelimisha wakulima wa pamba kanuni bora za kilimo hicho ili waweze kulima kwa tija na kuongeza uchumi wa mkulima, wilaya na taifa kwa ujumla. Uhamasishaji huo umefanyika kwa siku 5 katika Wilaya ya Maswa.
Halmashauri ya wilaya ya maswa ina majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Maswa Mashariki na Maswa Magharibi yenye Kata 36, Vijiji 120 na Vitongoji 510 wakulima wa pamba katika Wilaya ya Maswa wapo zaidi ya 92,000 ambao kwa wastani wanalima heka 1 na kuendelea.
Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha Pamba kwa wingi hivyo kwa umuhimu huo serikali imeagiza Mkoa wa Simiyu kufikia 2025 iwe na uwezo wa kuzalisha Tani zipatazo 500,000 za pamba na Wilaya ya Maswa inatakiwa kuzalisha Tani 130,000 ifikapo mwaka 2025 kwa kuwa ni Wilaya ya pili kimkoa inayozalisha pamba kwa wingi.
Ili kutilia mkazo katika zao hilo bodi ya pamba Tanzania chini ya balozi wake Mhe. Agrrey Mwanri imemlika katika Wilaya hiyo ya Maswa kuongeza nguvu kwa kutoa Elimu ya kanuni bora za kilimo cha pamba ambazo zitaongeza tija katika kilimo hicho na kumfanya mkulima kuzalisha kilo 2,000 kwa heka moja endapo atafata kanuni bora za kilimo cha kisasa cha zao la pamba ambalo litamwinua mkulima katika uchumi wake na kuongeza mapato ya Wilaya, mtu, kaya na familia kwa ujumla.
Kuna hatua mbalimbali ambazo mkulima anatakiwa kupita katika uzalishaji wa zao hilo la pamba.
Namna ya kuandaa shamba la pamba
Ng'oa masalia yote ya pamba ya msimu uliopita na ukusanye katikati ya shamba na kuyachoma moto hii itasaidia kuepukana na wadudu wote kama vile chawajani katika msimu mwingine wa kilimo.
Lima shamba lako mapema na tarehe ya kuanzia kupanda ni mwezi novemba tarehe 15 mpaka disemba 15 ili kuepusha pamba yako kuingiliwa na wadudu wakati wa ukame wa kuanzia mwezi Januari.
Lima shamba lako baada ya siku 3 vuruga tena au Lima shamba hilo tena tayari kwa kupanda mbegu kwa kuwa litakuwa limepoa.
Tumia vipimo vya kisasa vya kilimo cha pamba ambavyo ni sentimita 60 mstari kwa mstari au pima rula mbili ambayo itakuletea sentimita hizohizo 60, na sentimita 30 mche na mche au rula moja hii itasaidia mkulima kupata Miche 44,000.
Chimba shimo kwa kutumia ncha za jembe na sio jembe lote hii itasaidia mbegu yako kuota vizuri.
Weka mbolea ya samadi au DAP katika shimo ulilochimba na sio kuimwaga tu shambani hiyo itasaidia kutunza unyevu unyevu wakati wa ukame.
Fukia kidogo mbolea yako ili isigusane na mbegu yako kwa kuwa ikigusana itasababisha kuungua kwa mbegu uliyopanda.
Panda mbegu yako ya pamba kwa kila shimo mbegu 3-5 itasaidia kupata mbegu bora zaidi pia kusaidia mbegu kutoka kwa urahisi kuliko ile ambayo utaweka mbegu zaidi ya Tano hautapata mbegu nzuri na itakupotezea muda mwingi kupunguzia.
Mkulima epuka kuchanganya pamba na mazao mengine wakati unapanda mbegu za pamba, hii itasaidia kuepusha wadudu kushambulia pamba yako mfano kivuli cha mahindi hufubaza pamba na hivyo hutopata mavuno mengi.
Fukia mbegu yako na ni muhimu kuandika tarehe ya siku uliyopanda mbegu ya pamba.
Mbegu itaota baada ya siku 7 mkulima unatakiwa utembelee shamba lako ili kuona sehemu ambapo haijaota ili urudishie mbegu na sio mche.
Baada ya siku 21 punguzia Miche ibaki 2 tu ambayo itakuwa na rangi ya zambarau na kijani kinachovizia hiyo ndio pamba inayostahili kubaki shambani maana imekidhi vigezo vyote.
Hatua ya palizi
Kuna aina mbili za palizi ambazo ni palizi nzuri na palizi mbaya
Palizi nzuri ni Ile ambayo imekidhi vigezo vya kanuni bora za kilimo cha pamba kwa kufuata vipimo vya sentimita 60 kwa mstari na sentimita 30 mche na mche kuweka mbolea, na nafasi ya kupita wakati wa kupalilia.
Faida za palizi nzuri
Itasaidia kuongeza ubora wa pamba yako
Itazuia mmomonyoko wa ardhi
Itasaidia kufubaza magugu na nyasi kupata katika pamba
Palizi mbaya
Hii ni palizi ambayo haijakidhi kanuni za kilimo bora cha pamba mfano kumwaga mbegu, kutokuweka mbolea na kutokuchimba mashimo.
Athari za palizi mbaya
Husababisha mmomonyoko wa ardhi
Haizalishi Miche mingi
Palizi ya kutumia jembe la wanyamakazi hili ni jembe linalopalilia heka kuanzia 5 kwa siku na inashauriwa mkulima aliyefata kanuni za kilimo bora cha pamba ndio ataweza kutumia ili kurahisishia kazi na linapatikana katika bodi ya pamba hivyo kwa mkulima yeyote anayehitaji aandikishe jina lake kwa afisa ugani wa eneo lake.
Jinsi ya kunyunyuzia
Mkulima wa pamba unashauriwa kuwa endapo utaona wadudu katika shamba lako ni muhimu uchukue hatua za kunyunyuzia sumu katika pamba yako ili kuepusha pamba yako kuliwa na kupunguza uzalishaji.
Namna ya kunyunyuzia pamba
Pampu zilizotumika katika kampeni ya kutoa Elimu/ kuhamasisha wakulima kanuni bora za kilimo cha kisasa katika kipengele cha unyunyuziaji kulikuwa na aina mbili za pampu ambazo zilitumika ni pampu aina ya MATABI na pampu aina ya ULVA PLUS hizi ndizo pampu zilizotumika kutolea elimu kwa vitendo.
Jinsi ya kuchanganya sumu
Sumu inachanganywa kutokana na ujazo wa sumu ukoje katika chupa maana kila sumu ina ujazo tofautitofauti hivyo mkulima unashauriwa kuangalia katika chupa/ vifungashio hivyo vina milimita ngapi ndio uchanganye sumu yako kwa kufuata utaratibu.
Mfano katika elimu hiyo balozi wa pamba alitumia sumu aina ya charisma yenye mills 100 ambayo mkulima unatakiwa kugawa mara 3 hivyo utaweka mills 33 kwenye hizo Lita 2 za maji uliyoweka kwenye pampu.
Kisha tikisa mpaka dawa ichanganyike baada ya hapo weka Lita 14 za maji zilizobaki ili kukamilisha Lita 16 tikisa tayari kwa kunyunyuzia.
Mkulima unashauriwa kunyunyizia juu ya mmea na chini ya mmea ili kuua wadudu wote.
Pampu aina ya kadogoo/ Ulva plus hii ni aina ya pampu inayotumia betri nane ambayo inatumika kunyunyuzia pamba kwa njia ya mvuke tu.
Jinsi ya kutumia
Weka Lita 5 za maji
Weka sumu yote katika maji Kisha changanya
Nyunyuzia sumu juu tu kwa kuhesabu mistari 3 kisha mstari wa katikati ndio utapiga sumu yako ambayo itasambaa kwenye mistari mingine 2.
Angalizo
Mkulima unashauriwa kupiga sumu kuanzia saa mbili au saa tatu asubuhi kwa kuwa alfajili bado kuna umande mwingi hivyo wadudu hawatakufa kwenye pamba yako na pia ikifika saa 6 mchana ailisha zoezi hilo mpaka saa 11 jioni ambapo wadudu watakuwa wanaonekana hivyo ni vizuri mkulima wa pamba kuzingatia hilo.
Mkulima anashauriwa kutumia nozeli ambayo ni maalumu kwa pamba na sio kila nozeli ni nzuri kwa matumizi ya kupulizia kwenye pamba.
Jinsi ya kuvuna pamba
Wakati wa kuvuna pamba mkulima wa pamba anatakiwa kuvuna vizuri pamba yake na kuihifadhi kwenye mifuko maalumu ambayo itatolewa na bodi ya pamba bure kabisa ili pamba hiyo ipate soko zuri kimataifa.
Balozi wa pamba amefika Wilaya ya Maswa na kutoa elimu kwa vitendo ya kanuni bora za kilimo cha pamba. Takribani wakulima zaidi ya 5,155 kutoka katika Kata 11 kati ya 36 Vijiji 30 kati ya 120 walitembelewa.
Wakulima wa Maswa wamefurahia elimu hiyo kwa kuwa itawaletea manufaa na wamemshukuru sana balozi kwa kujitoa kwake kufika Maswa na kuwaelimisha kwa vitendo kanuni bora za kilimo cha pamba na wameahidi watazingatia yote waliyoelekezwa ili wapate pamba nyingi.
Mtaalam akionyesha namna ya kuchimba mashimo kwa kutumia ncha ya jembe
Mtaalam wa Kilimo pamoja na mkulima maarufu wakionyesha jinsi ya kushika mbegu wakati wa kupanda
Mkulima akionyesha namna ya kupalilia kwa kutumia jembe la wanyamakazi katika shamba
Balozi wa pamba akitoa elimu ya unyunyuziaji kwa kutumia pampu aina ya MATABI
Balozi wa pamba akitoa elimu ya kunyunyuzia kwa kutumia pampu aina ya ULVA PLUS katika zao la pamba
Balozi akitoa elimu ya jinsi ya kutumia mifuko ya kuvunia na kuhifadhia pamba wakati wa kuvuna pamba
Mkulima wa pamba akimshukuru balozi wa pamba kwa elimu nzuri waliyoipata ya kanuni bora za kilimo cha pamba
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.