Katibu Tawala Wilaya ya Maswa ndg Agness A. Alex amezindua rasmi timu ya usimamizi wa ununuzi wa zao la pamba msimu wa 2023 ngazi ya Wilaya yenye jukumu la kusimamia ununuzi wa pamba usafirishaji, kukusanya takwimu za pamba, kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa ununuzi pamoja na kuhakikisha taratibu, sheria na kanuni za ununuzi wa zao la pamba zinafatwa kwenye soko.
Katibu tawala ameyasema hayo wakati akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya leo tarehe 30.05.2023 na kuhudhuriwa na kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, timu ya usimamizi wa pamba (task force), Afisa utumishi na watendaji wa Kata.
Ndg Alex ameitaka timu hiyo ya usimamizi wa pamba ifanye kazi kwa weredi, utiifu na uaminifu ili kusimamia mapato kwa kuwaongezea nguvu watendaji ili kuthibiti mianya ya upotevu wa mapato na pia ameiomba timu hiyo kuepuka kuchukua rushwa wakati wakitimiza majukumu yao kwa kuwa wameaminiwa na wilaya kufanya kazi hiyo.
Aidha Katibu tawala amewataka watendaji wa kata kusimamia na kupita kila wakati kukagua katika mageti hayo ili kuona namna ambavyo kazi inafanyika ya usafirishaji wa pamba
Awali akisoma taarifa hiyo Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Robert Urassa amesema mageti 15 yameanzishwa ambayo magari yatakuwa yanapita na yakiwa na kibali cha kusafirisha pamba.
Pia amewataka watendaji wa kata kuwahimiza watendaji wa vijiji kuwepo katika maeneo ya ofisi za wanunuzi wa pamba ikiwepo vituo binafsi na AMCOS ambapo zitasaidia kupata taarifa za Kila siku ya zoezi la ununuzi linaloendelea Katika wilaya ya Maswa ili wawasilishe kwa watendaji wa Kata.
Kwa upande mwingine Katibu Tawala amewataka watumishi kuzingatia kanuni, taratibu, Sheria na muongozo wa mavazi ya utumishi wa umma kwa kuenenda kama mtumishi sambamba na kutunza vifaa walivyopewa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kikazi na sio kutumia kwa mambo Yao binafsi kama vile bodaboda.
Pia Ndg Alex amewashauri watumishi kuwa na nidhamu pamoja na kushirikiana kwa kubadilishana mawazo hiyo itawasaidia watumishi hao kuwa na ufanisi katika kazi kwa kuwa wataweza kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili.
Vilevile Katibu Tawala wa wilaya amewataka watendaji wa Kata kuhamasisha wananchii katika kata zao kufika katika miradi ambapo Mwenge wa uhuru utakapopita uwakute ili waone Mwenge wa Uhuru unavyokagua miradi ambayo Serikali inatekeleza katika Wilaya ya Maswa.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.