Leo tarehe 10/4/2019 kimefanyika kikao cha tathmini ya taaluma Wilayani Maswa. Kikao hiki kimehusisha Walimu wakuu, Wakuu wa shule, Walimu mahiri Wilayani hapa, Maafisa elimu Kata, Viongozi wa Elimu ngazi ya wilaya na Mkoa. Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Dr. Seif Shekarage.
Mgeni rasmi amewashauri walimu kulenga mbali kama wanataka kufanikiwa, hii ni kulenga kufaulisha wanafunzi wote na kushika nafasi nzuri kitaifa. Katika suala zima la tathmini imeshauriwa tathmini ianze kufanyika tangu kwa Mwalimu wa Somo.
Pia ameshauri Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule wazieleze Kamati na Bodi za Shule kusimamia suala la upatikanaji wa chakula cha wanafunzi shuleni kwa kupitia uhamasishaji wa wazazi kuchangia. Wasimamie changamoto ya utoro katika shule zao ikiwa ni pamoja kuorodhesha majina ya Watoto watoro na kuyapeleka kwa afisa Mtendaji wa Kijiji/Kata na siyo Mwalimu kufuatilia hao watoro mwenyewe.
Amewaasa Walimu wasijihusishe na Wanafunzi katika suala la mapenzi kwani ni hatari katika maisha ya kazi yao. Pia ametoa ushauri kwa Walimu kuepuka mikopo isiyokuwa ya lazima kwani inawasababishia matatizo katika familia zao na kuwakosesha amani ya ufanisi wa kazi zao. Kwa msisitizo amesema "Kopeni kwa mpango na katika taasisi za kifedha zinazotambulika"
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa amewaasa Wakuu wa Shule na Walimu wakuu kusimamia suala la nidhamu kwa ujumla katika shule zao kwa kufanya vikao na kuwaelimisha walimu ili kuondoa ombwe la walimu kuingia kwenye matatizo yasiyo ya lazima yanayowasababishia wengine hata kufukuzwa kazi.
Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu ametoa mwongozo wa jinsi gani ya kuboresha elimu kuanzia ngazi ya shule hadi Wilaya. Zinatakiwa kuwepo kamati za taaluma kuanzia ngazi ya shule hadi Wilaya. Kamati hizi zitajumuisha Walimu mahiri wa masomo.
Katibu wa Chama cha walimu Mkoa wa Simiyu amewakumbusha Walimu haki na wajibu wa majukumu yao katika maeneo ya kazi. Aidha ametoa zawadi kwa shule zilizoongoza kwenye matokeo na zilizo kuwa za mwisho. Ametoa zawadi kwa Shule ya Msingi Mwanundi kg.5 za Sukari, Shule ya msingi Nyanguganwa kg.25 za sukari, Shule ya Sekondari Budekwa kg.10 za sukari na Shule ya Sekondari Senani kg.25 za sukari.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.