Serikali kupitia mfuko wa TASAF imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali Wilayani Maswa ambapo Kijiji cha Mwabujiku kilichoko Kata ya Zanzui kimenufaika kwa kupata kiasi cha Tshs. 7,674,545. 54 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Vyumba 2 vya Madarasa, Choo matundu sita (6) na Ofisi ya Walimu moja (1).
Akizungumza na wananchi katika mkutano mkuu wa Kijiji cha Mwabujiku uliofanyika leo tarehe 20 April 2022 wenye lengo la kuhamasisha wananchi kujitolea nguvu kazi katika mradi huo, Afisa Ufuatiliaji TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg John Wambura amempongeza Mh. Diwani kwa kuupigania huo mradi na amewaomba wananchi kujituma zaidi kwa sababu bado wapo nyuma. Na lengo la TASAF ni kuona mradi unakamilika kwa wakati .
Pia Afisa huyo ameongeza kuwa kuanzia tarehe 27 April 2022 kutakuwa na mafunzo ya siku tatu 3 katika Kata ya Zanzui ambayo yatahusisha wajumbe wa kamati ya CMC kutoka Mwabayanda na Zanzui yenye lengo la kuweka mikakati ya utekelezaji wa mradi huo.
Aidha Wambura amewasihi wanakamati wa CMC wasiwe na tamaa katika fedha hizo wawe waaminifu na wawazi ili mradi huo ukamilike kwa ubora unaotakiwa na amemuomba Mhe. Diwani kufuatilia kwa karibu utekelezaji huo kwenye suala la fedha.
Awali akiwasilisha taarifa Afisa Maendeleo ya Jamii Ndg. Berther Lugenji amewaomba wananchi kutoa ushirikiano mkubwa wa nguvu kazi ili mradi ukamilike na fedha hizo zisiweze kuhamishwa na kupelekwa sehemu nyingine kwa sababu serikali imetoa asilimia 90% kwenye mradi huo na wananchi wanatakiwa kuchangia asilimia 10% katika mradi huo kama ambavyo mlivyokubaliana katika kikao Cha mwanzo .
Kwa upande wake Ndg. Donatus Weginah Afisa Mipango wa Mkoa wa Simiyu ameelezea jinsi ambavyo wananchi wenyewe waliibua miradi hiyo kutokana na mahitaji waliyokuwa nayo na serikali imetimiza wajibu wake wa kutoa fedha ili kusaidia utekelezaji wa mradi huo na amewaomba wananchi kujitoa kama makubaliano yalivyokuwa.
"Wajibu wa msingi ni upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ambavyo vipo katika maeneo yetu vifaa hivyo ni mchanga, kokoto, mawe, maji pamoja na nguvu kazi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa muda uliopangwa” amesema Donatus
Aidha Diwani wa kata ya Zanzui Mh. Jeremia Mange Shigala ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hasan kwa kuwaletea fedha katika Kijiji Cha Mwabujiku kupitia mfuko wa TASAF ili wapunguze changamoto hizo za madarasa na vyoo katika Kijiji hicho na amewaomba Mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji kutoa ushirikiano kwa wananchi katika zoezi hilo ili mradi ukamilike kwa wakati na waweze kuletewa miradi mingine.
Kwa upande wao wananchi wameupokea mradi huo na wameahidi kushiriki kikamilifu katika kazi hiyo na tayari wamepeleka mchanga katika eneo ambalo mradi utafanyika tayari kwa utekelezaji ili kuwasaidia watoto wao kupata mazingira mazuri ya kusomea.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mwabujiku Mwl. Mariam Ngowi ameishukuru TASAF kwa kupeleka mradi huo katika shule yake wa madarasa hayo mawili , choo matundu sita (6) na ofisi ya walimu itawasaidia kupunguza changamoto zilizopo hapo shuleni kwa sababu Madarasa waliyonayo Sasa hivi hayatoshelezi mahitaji ya wanafunzi katika shule hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.