Umoja wa Walimu Wakuu Wilaya ya Maswa wamefanya uchaguzi na kupata viongozi wapya ambao wataongoza Umoja huo kwa muda wa miaka mitano kwa mujibu wa kanuni za umoja huo.
Lengo la chombo hicho ni kuhakikisha kinasimamia taaluma na kushirikiana na ofisi ya mkuu wa divisheni ya elimu ya awali na elimu msingi wilaya kwa ajili ya kukuza taaluma.
Nafasi zilizokuwa zinagombewa ni Mwenyekiti wa TAPSHA Wilaya ya Maswa, Mwenyekiti Msaidizi, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi na Mhasibu wa TAPSHA Wilaya ya Maswa ambapo katika uchaguzi huo nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu walipita bila kupingwa kwa kuwa hapakuwa na wagombea zaidi ya wawili.
Katika Uchaguzi huo Mwl. Mbaga Shilla amechaguliwa kwa awamu nyingine kuongoza umoja huo wa walimu wakuu Wilaya ya Maswa, ambapo nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa TAPSHA ni Mwalimu Florence Mwita, Katibu Mkuu wa TAPSHA Wilaya ni Lucas Zitto na Mhasibu wa TAPSHA Wilaya ni Nyanswi Samwel.
Nafasi iliyopigiwa kura ilikuwa ni nafasi ya mhasibu ambapo kulikuwa na wagombea wawili ambao ni Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyalikungu Mwalimu Nyanswi Samwel na Mwalimu mkuu shule ya msingi Ngongwa Mwl Advera Charles.
Katika kinyang’anyilo hicho wapiga kura walikuwa 98 na Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyalikungu aliibuka kidedea kwa kupata kura 64 dhidi ya mpinzani wake aliyepata kura 34 na kutangazwa na Mwenyekiti wa Uchaguzi kuwa Mhasibu wa TAPSHA Wilaya ya Maswa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Uchaguzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa TAPSHA Mkoa Mwl. Marco Manyenye amesema katika nafasi ya Katibu Msaidizi mgombea alipungukiwa sifa kwa mujibu wa kanuni za TAPSHA.
Baada ya ushindi huo viongozi hao wamewashukuru viongozi wenzao kwa kuwaamini na kuwachagua ili waweze kuwaongoza na pia wameahidi kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano umoja na kushauriana ili kujenga TAPSHA yenye nguvu na kuinua taaluma mashuleni.
Aidha Mwenyekiti wa TAPSHA Wilaya ya Maswa baada ya kuchaguliwa amesema Umoja na ushirikano ndio utakaoufanya umoja huo kufanya kile ambacho kimekusudiwa ili kuleta tija katika taaluma.
Akimwakilisha mlezi wa TAPSHA Wilaya ya Maswa ambaye pia ni Afisa Elimu msingi Wilaya ya Maswa, Afisa Taaluma Wilaya ndugu Joseph Omahe amewapongeza viongozi kwa kupata nafasi hiyo na amewaomba viongozi wa TAPSHA kuongeza kipengele kwa mgombea wa nafasi yeyote katika Umoja huo ahakikishe shule yake inafanya vizuri kitaaluma.
Pia ametoa wito kwa viongozi hao kusimamia taaluma na sio kuangalia maslahi yao binafsi bali wawe viongozi ambao watasimamia taaluma ya watoto ambao hawajajitambua.
Awali katibu wa TAPSHA Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mwalimu mkuu shule ya Sangaitinje Wilaya ya Meatu amewapongeza Walimu Wakuu kwa kuitikia wito wa kuchagua viongozi ambao watasukuma gurudumu la TAPSHA kwa muda wa miaka mitano mingine kwa mujibu wa katiba.
Pia amesema TAPSHA ndio sauti ya Walimu Wakuu kwa kuisaidia serikali na kuisaidia Ofisi ya Afisa Elimu Msingi kuhakikisha kwamba wanasonga mbele kitaaluma.
"Niwaombe viongozi wenzangu kwa zoezi ambalo liko mbele yetu wapo viongozi ambao wamemaliza muda wao tumeona utendaji wao wa kazi tunakwenda kuchagua viongozi wengine tusichague viongozi kwa mhemuko, tusichague viongozi kwa kuangalia kwamba flani kafanya nini bali tuangalie atatufikisha wapi kwa upande wa taaluma"
Pia amesema viongozi hao wakiitumia vizuri TAPSHA itawasaidia kujifunza kwa majirani, wao kwa wao namna bora ya ufundishaji na hata wengine wanafanyaje kupata matokeo mazuri, pamoja na kutatua changamoto zinazowahusu wao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.