Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Labani Kihongosi amepiga marufuku wanasiasa kugawa mbegu na mbolea kwa wakulima na kuwataka wajikite Zaidi kwenye kazi zao za siasa.
Mhe Kihongosi alisema hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata za Mpindo, Senani, Ipililo na Nguliguli zilizopo wilayani Maswa Mkoani Simiyu.
Ameongeza kuwa jukumu la ugawaji wa mbegu na mbolea linatakiwa kusimamiwa na wataalamu wa kilimo ili kuepusha upotevu wa mbegu na mbolea zinazotolewa kwa wananchi ili ziwanufaishe wakulima.
“Mtu hana shamba, mtu halimi pamba, mtu hafanyi lolote unakuta anapewa mbegu na mbolea madhara yake anaenda kuuza wakati kuna mkulima anatakiwa apate mbegu na mbolea ili akazalishe aweze kupata mafanikio.” Ameeleza Mkuu wa Mkoa.
Aidha Mhe Kihongosi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya kununua mbegu na mbolea kwa wananchi ili wanufaike na wapate faida kupitia kilimo.
Sanjali na hilo Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa viongozi wa AMCOS kuwatendea haki wakulima na kusimamia haki zao na sio kujinufaisha wao wenyewe.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.