Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda amewataka wananchi wa Maswa na wilaya jirani kuchangamkia fursa za zana za kilimo ambazo zitawasaidia katika shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji.
Dkt Nawanda amesema hayo akiwa katika kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMERTEC) kilichopo kijiji cha Mwandete Kata ya Sangamwalugesha wakati akitembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Mkuu wa mkoa amesema kuwa wananchi wa Maswa wanatakiwa wafike katika kituo hicho ili kupata mafunzo ya teknolojia mpya, ushauri na kukodi zana hizo ili ziwasaidie katika kujiongezea kipato.
Pia Mkuu wa Mkoa amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwapeleka vijana wanaojishughulisha na kilimo kufika katika kituo hicho cha zana za kilimo ili waweze kujifunza mbinu bora za kutumia teknolojia mpya ya zana za kilimo zitakazowasaidia kulima kwa tija ili kupata mazao mengi.
Kwa upande wake Mhe. Diwani wa Kata ya Sangamwalugesha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupeleka kituo hicho katika Kata yake kwa kuwa kimekuwa msaada mkubwa katika eneo lake kwa wakulima na wafugaji pia amewataka wananchi kutoka Kata zingine kufika katika kituo hicho ili kupata ujuzi kuhusu zana hizo za kilimo.
Kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali zikiwepo mashine za kupura mazao mbalimbali kama vile Mahindi, Mtama, Karanga na Alizeti, huduma ya uwekaji wa vifaa vya gesi asilia inayotokana na kinyesi cha wanyama, matela ya kubebea mizigo, mashine za kupandia mazao na mashine za kukatia viazi (michembe).
Akiwa Wilayani Maswa Mkuu wa Mkoa ametembelea kikundi cha vijana Maswa Diagnostic Centre kilichopo Shanwa kinachojishughulisha na utoaji wa huduma ya upimaji ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni 16 ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa ajili ya kutoa huduma ya vipimo vya magonjwa mbalimbali ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali na vituo vya afya.
Aidha ametembelea kiwanda cha mjasiriamali Liliani Kinyemi (ABC) ambacho kinashirikiana na Halmashauri kwa ajili ya kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi, mchele na ulezi kwa kuongeza virutubishi aina ya zinki, chuma, foliki asidi na vitamin B12 ambavyo vitawasaidia watoto wanaozaliwa kuzuia utapiamlo na kupunguza udumavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Pia amekagua tenki la maji katika Kata ya Nyalikungu lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni moja, ujenzi wa shule mpya ya msingi katika Kata ya Jija, ujenzi wa shule mpya ya msingi katika Kata ya Shishiyu na kituo cha afya Badi.
Dkt Nawanda amempongeza Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha nyingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi mpya, vituo vya afya, matenki ya maji na barabara.
Kwa upande wa wananchi wamemshukuru Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutoa Fedha ambazo zimewezesha kujenga miundombinu mbalimbali yenye lengo la kuwasaidia wananchi kupata huduma hizo kwa uhakika ikiwepo vituo vya Afya, Shule na Maji.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.