Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya Wilaya mpaka Kijiji kuhakikisha wanahamasisha Usafi wa Mazingira katika maeneo yote ya kazi na makazi ili kuepukana na ugonjwa wa kuhara na kutapika.
Dkt Nawanda ametoa agizo hilo katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa, mganga mkuu wa Mkoa, mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Maswa, wakuu wa Divisheni, kamati ya CHMT ya Wilaya, Maafisa Tarafa, watendaji wa Kata na vijiji, wazee maarufu na viongozi wa dini.
"Viongozi wa dini pamoja na wazee maarufu Mimi nawaombeni sana Kila mmoja katika eneo lake aende akahamasishe Usafi wa Mazingira. Mimi ninaamini viongozi wa dini pamoja na ninyi wazee mkisema huu ugonjwa basi hapa Maswa hakuna mtu atakayehara Wala kutapika Mimi nimekuja hapa kuhamasisha Usafi wa Mazingira." Amesema Dkt Nawanda
Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku wananchi kula chakula katika mikusanyiko ya watu kama vile msibani, pia ametoa wito maeneo yote ya migahawa yanatakiwa kuwa na maji ya kuchemshwa yaliyowekwa kwenye ndoo, sambamba na hilo ametoa zuio kwa wafanyabiashara wa mahindi ya kucheshwa kuuzwa maeneo ya stendi.
"Sehemu zote za kuuza pombe za kienyeji zisizo na vyoo zote ni marufuku na mpige fullstop kuanzia Leo hii kwa sababu ya mtu akilewa hachagui sehemu ya kwenda haja." Amesema Dkt Nawanda
Aidha amewataka viongozi wa MAUWASA na RUWASA kutoa huduma ya maji bure katika maeneo yote yaliyoathirika na tatizo la kuhara na kutapika kwa kipindi Cha mwezi mmoja na kutibu maji hayo kwa kutumia dawa katika visima vilivyochimbwa na wananchi binafsi ili wananchi wasiwe na kisingizio cha kutokupata maji safi na salama.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge amesema baada ya kupata taarifa 27 Disemba 2023 kuwa Kuna ugonjwa wa kuhara na kutapika timu za ufatiliaji ziliundwa lengo likiwa ni kutoa elimu na kuhakikisha wananchi wanakuwa na vyoo bora na wanavitumia .
"Kwa ambao hawana vyoo tulisisitiza timu hizo kuanzia ngazi ya Wilaya, Kata na Kijiji kutoa elimu kwa wananchi pale ambapo imeshindikana watu hawajatii elimu na kuzingatia basi hatua za kisheria zichukuliwe kwa wananchi hao. Na tayari hatua hizo zimeanza kuchukuliwa."amesema Mhe Kaminyoge
"Tumefanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na Maafisa kutoka Wizara ya Afya wapo lakini tumepata ushirikiano mkubwa wa Maafisa kutoka ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wetu wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya Kila siku tunao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba ugonjwa wa kuharisha tunautokomeza na usiendelee kuathiri wananchi wetu." Amesema Mhe Kaminyoge
Pia Mkuu wa Wilaya amesema mikakati imewekwa ambapo suala kubwa ilikuwa ni kuwaelimisha na kuwasisitiza wananchi kufata kanuni za afya kupitia kamati ya afya ya wilaya.
Mkuu wa Mkoa akiwa wilayani Maswa amekagua kaya 12 katika Kata ya Shanwa ili kuona Usafi wa Mazingira ulivyo katika maeneo hayo hasahasa vyoo wanavyovitumia wananchi katika kaya zao na maeneo ya biashara.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.