Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda amechangia mifuko 50 ya simenti kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari Malampaka ambayo majengo yake yamejengwa kwa ubora zaidi ya majengo mengine.
Nawanda amesema wilaya ya Maswa imepewa zaidi ya shilingi bilioni 30 na serikali ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Maswa ikiwa bilioni 3 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ambayo itakuwa na mabweni.
Amesema hayo katika stendi ya Malampaka wakati akizungumza na wananchi wa Malampaka na kusikiliza kero zao na kuwaeleza wananchi miradi mbalimbali inayotekelezwa na ambayo imetekelezwa katika wilaya ya Maswa ikiwepo mradi wa reli ya kisasa ambapo makao makuu yatakuwa Malampaka hivyo itakuza uchumi na kuongeza mapato ya Wilaya pamoja na mwananchi mmojammoja.
Dkt Nawanda amesema zao la pamba ni muhimu sana na Mkoa wa Simiyu unatakiwa kuzalisha Tani 300,000 za pamba kwa mwaka huu hivyo amempongeza balozi wa pamba Tanzania Mhe Agrrey Mwanri ambaye yupo wilaya ya Maswa kwa kutoa Elimu nzuri ambayo wakulima wa pamba wanatakiwa kufata kwa kuwa katika Mkoa wa Simiyu Tani 500,000 zinatakiwa kuzalishwa ifikapo 2025.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema balozi wa pamba amesaidia kutoa Elimu nzuri kwa wakulima ambayo itawasaidia kutumia vipimo vya sm.60 kwa kila mstari na sm.30 kwa kila mche, kuchoma mabaki yote ya pamba ya msimu uliopita, na kuwataka maafisa ugani wote kuwa na shamba ili iwe mfano mzuri kwa wakulima wote kujifunza kwao.
Pia Mkuu wa mkoa amewasisitiza wananchi kuwaamdikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule kwa Elimu ya awali na msingi muhula wa 2023 waandikishwe ili kujua idadi ya watoto hao katika Wilaya ya Maswa na Mkoa mzima wa Simiyu pia amewataka wananchi wote kuchangia chakula shuleni ili ufaulu wa wanafunzi uongezeke.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya amempongeza Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kuleta zaidi ya shilingi bilioni 35 ya miradi mbalimbali ikiwepo Zahanati, Vituo vya Afya, Barabara, Umeme na Maji.
Mkuu wa Mkoa yupo Maswa kwa ziara ya siku tatu kutembelea miradi katika Tarafa tatu na ameambatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa, wakuu wote wa taasisi, wakuu wa idara, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Maswa.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.