Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius John Ndejembi amefanya ziara wilayani Maswa mkoani Simiyu katika Kata ya Budekwa kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Budekwa linalojengwa na serikali kupitia mpango wa TASAF OPEC IV
Akizungumza na wananchi na wanafunzi leo tarehe 28.9.2022 katika eneo hilo la mradi Naibu Waziri amewataka watumishi wote na wananchi kusimamia kwa karibu mradi huo kwa kuwa mradi huo upo nyuma ya wakati kwa kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha kwa wakati mradi huo ambao utasaidia kuwalinda watoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni.
Aidha Mhe. Ndejembi amewaomba wananchi kujitoa kikamilifu ili kukamilisha miradi ya maendeleo kwa kuwa serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Samia Suluhu Hasani imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo amewasisitiza watendaji wote kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa na Wilaya kuwa na uchungu na kazi wanazozifanya ili serikali iendelee kuleta fedha kwenye miradi mingine.
Awali akisoma taarifa hiyo kwa Naibu Waziri Afisa Mtendaji wa Kata ya Budekwa Ndg. Masesa Madirisha amesema mradi huo wa bweni la wasichana utagharimu Tsh. 168,399,000/= ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 80, ambapo TSh. 150,356,250/= ni fedha kutoka makao makuu TASAF na pesa zingine ni kutoka kwa wananchi ambao walichangia Tsh. 18,042,750/= kwa ajili ya malighafi mchanga, mawe, maji na uchimbaji wa msingi na Halmashauri ilichangia tripu 10 za kokoto zenye thamani ya Tsh. 2,800,000/= mradi huo ukikamilika utasaidia watoto wa kaya maskini na kupunguza mimba za utotoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Simon Berege amesema maelekezo yote ameyapokea kutoka kwa Naibu Waziri na kuahidi kuongeza kasi katika mradi huo ambapo kazi hiyo itafanyika usiku na mchana ili mradi uweze kukamilika kwa wakati pia amemweleza Mhe. Naibu Waziri kuwa Wilaya ya Maswa imepokea Tsh. Milioni 600 kwa ajili ya miradi mingine.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.