Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Abdalla Shaib Kaim ameipongeza Wilaya ya Maswa iliyopo Mkoa wa Simiyu kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo kwa sababu Mwenge wa Uhuru umepita katika miradi hiyo na kuridhishwa nayo kwa kuwa imetekelezwa kwa ufanisi na weredi.
Akiwa wilayani Maswa Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa amezindua jengo la Wagonjwa wa nje, mama na mtoto, katika Zahanati ya Nguliguli katika Kata ya Lalago ambapo mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 271 ambazo zimetolewa na serikali kupitia mfuko wa global fund.
Zahanati hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 17,079 ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kutatafuta huduma hiyo sambamba na hilo, pia amegawa vyandarua kwa makundi maalumu ambayo ni mama wajawazito wazee na watoto chini ya miaka mitano.
Aidha Ndg Kaim ameweka jiwe la msingi ujenzi wa Bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mwagala lililopo Kata ya Lalago lenye thamani ya Shilingi milioni 114 ambapo Fedha hizo zimetolewa na serikali kupitia mradi wa EP4R, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa pamoja na nguvu za wananchi ambapo ujenzi wake upo katika hatua za ukamilishaji.
Pia kiongozi wa Mwenge wa uhuru amepanda mti katika bweni hilo, kuzindua klabu ya wapinga rushwa na kutoa cheti katika shule ya sekondari Mwagala, kukagua na kuona utoaji wa Elimu ya lishe inayozingatia makundi matano ya vyakula kwa njia ya kupika vyakula vyenye lishe bora.
Katika hatua nyingine Ndg. Kaim amezindua mradi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa Lita milioni moja na mfumo wa usambazaji maji katika Kata ya Nyalikungu wenye thamani ya bilioni 1 tenki hilo ambalo litasambaza maji katika vitongoji 25 kati ya 40 vya mji wa Maswa na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Wilaya ya Maswa.
Vilevile kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa ametembelea na kuona vifaa tiba vinavyotumika katika shughuli za kimaabara katika kikundi cha vijana kilichopo katika Kitongoji cha Kumalija Kata ya Shanwa, kikundi hicho kimeanzisha Maabara yenye thamani ya shilingi milioni 18 ambayo wamewezeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kupatiwa kiasi Cha shilingi milioni 16 kutoka asilimia 10 na wao kutoa kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya kutoa huduma ya vipimo vya magonjwa mbalimbali ili kupunguza msongamano katika vituo vingine vya kutolea huduma za Afya.
Mradi ambao utawasaidia vijana kiuchumi kwa kujiajiri na kuajiri wengine kwa lengo la kujipatia kipato na kusogeza huduma karibu kwa wananchi ambapo vipimo vinavyotolewa hapo ni upimaji wa tezi dume na vipimo vingine vingi.
Ndg. Kaim amewapongeza vijana hao kwa kuwa na moyo wa kizalendo ubunifu na weredi kwa kufanya jambo hilo ambalo limewavutia pia amewapa kongole Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kuwawezesha vijana hao Fedha ya mkopo wa asilimia 10 ili waweze kujiajiri wenyewe.
Pia kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kiatifa ametembelea na kuona utoaji wa Elimu katika kupambana na maabukizi ya VVU- UKIMWI na kuona namna Elimu inavyotolewa pamoja na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.