Wakazi 51 wa Kijiji Cha Malampaka kata ya Malampaka wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wamekosa makazi baada ya mvua kubwa ya upepo, iliyoambatana na mawe kunyesha na kusababisha nyumba za wananchi kubomoka pamoja na mapaa ya nyumba zao kuezuriwa.
Kutokana na maafa hayo Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amefika katika nyumba hizo pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ili kufanya tathmini ya vitu vilivyoharibika na kutoa pole kwa waathirika wote wa maaafa na kuona namna ambavyo wananchi hao watasaidiwa katika maradhi.
Mhe. Kaminyoge amewashauri viongozi wa vijiji kuwa karibu na wananchi waliopata maafa kwa kuwapa hifadhi na sehemu ambazo zinawezekana kurudishiwa wasaidie kurudishia.
Pia mkuu wa wilaya amemwagiza Mkurugenzi kupitia kamati ya maafa kuona namna ya kuwasaidia chakula wananchi hao waliokubwa na maafa.
“Serikali imetoa mahindi ya bei nafuu ningeomba Halmashauri ione hizi familia ambazo zimeathirika itoe angalau kilo 60 za mahindi kwa familia hizi, watafutiwe dagaa au maharage ili wasiangahike juu ya chakula, wahangaikie namna ya kurudisha makazi yao” amesema Mkuu wa Wilaya.
Kamiyonge amewashauri Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kupitia Divisheni ya Ujenzi kuwashauri wananchi kuboresha majengo yao kwa kuwa baadhi ya nyumba ambazo zimeathirika ni za muda mrefu hivyo kutohimili hali ya hewa ya aina hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Malampaka Mhe: Mashala Renatus Masalu amemshukuru mkuu wa Wilaya kwa kufika kwa wakati, kuwafariji na kuona namna ambavyo athari zimetokea kwa wananchi hao waliokumbwa na maafa .
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.