Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge ameziagiza taasisi zote za serikali kutunza miti yote iliyopandwa katika bonde la Mto Sola lengo kubwa likiwa ni kuhifadhi chanzo cha maji yanayokwenda kwenye bwawa la Zanzui.
Akizungumza katika eneo hilo la bonde la Mto Sola leo tarehe 2 Januari 2023 wakati wa zoezi la upandaji wa miti lililofanyika katika bonde hilo. Mhe Kaminyoge amesema suala la mazingira ni suala mtambuka hivyo kila taasisi ya kiserikali washirikiane katika kupanda miti mpaka tarehe 15 mwezi huu na kila taasisi iweke bajeti ya utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kutengeneza vitalu katika bwawa la Zanzui (New Sola) ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mkuu wa Wilaya amesema Afisa Mazingira ndio mwenye mamlaka ya kuibua ajenda za utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti wakati wa mwanzo wa msimu katika vikao na kwenye balaza la madiwani ili kujadili mustakabali wa suala hilo la utunzaji wa chanzo cha Mto Sola.
Pia Mkuu wa Wilaya amewataka watendaji wote wenye mamlaka katika eneo hilo kusimamia chanzo hicho cha maji ili shughuli zote za kiuchumi na kijamii zinazoendelea katika chanzo hicho zisitishwe mara moja. Na kiongozi yeyote atakayeshidwa kusimamia hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sola Mhe. Masanja Mpiga amempongeza Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa kazi kubwa anayoifanya ya usimamizi wa shughuli hiyo ya upandaji wa miti ili kulinda chanzo hicho cha maji ambacho kitasaidia upatikanaji wa maji na kuwaomba wataalamu wasaidie katika jambo hilo. Pia amewataka wananchi kutii sheria zilizowekwa katika bonde hilo na wawe walinzi wa maeneo ya vyanzo vya maji ili kuepukana na ukosefu wa maji.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe. Mary Misangu amesikitishwa na uzembe unaojitokeza katika Divisheni ya mazingira na maliasili kwa kuwa wao ndio wana mamlaka ya kusimamia chanzo hicho ili shughuli zozote za kiuchumi na kijamii zisiendelee lakini mpaka sasa tayari wananchi wamelima katika chanzo hicho hivyo amemuahidi Mhe. Mkuu wa Wilaya kushughulikia suala hilo.
Zoezi hilo limeshirikisha taasisi mbalimbali za serikali ambazo ni Halmashauri ya Wilaya, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mamlaka ya mji mdogo, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, Jeshi la akiba, Jeshi la magereza na watendaji wa Kata na Kitongoji cha uwanja wa ndege.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.