Mradi wa BOOST ni mradi ambao upo kwa ajili ya kuinua elimu ya Awali na Msingi, lengo kuu la mradi huu ni kuboresha upatikanaji wa fursa katika ufundishaji na ujifunzaji bora wa elimu ya awali na msingi katika ujenzi wa miundombinu ya elimu.
Kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya elimu hasahasa elimu ya msingi kuwa na uhaba wa madarasa ambapo inapelekea wanafunzi zaidi ya 200 au 150 kukaa darasa moja, upungufu wa vyoo na shule za Watoto wa chekechea, serikali ya awamu ya sita iliona changamoto hizo na kuja na mwarobaini wa kutatua changamoto hizo katika maeneo husika.
Halmashauri ya wilaya ya Maswa ni miongoni mwa Halmashauri zilizonufaika na mradi huo ambapo serikali ya awamu ya sita chini ya Rais shupavu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya kutatua changamoto na kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwepo ujenzi wa shule mpya 3, ujenzi wa matundu ya vyoo na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw. Maisha S. Mtipa ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Maswa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika idara ya elimu hasa upande wa elimu ya msingi.
Bw. Mtipa aliogeza kuwa fedha hizo zimejenga miundombinu mbalimbali katika majimbo yote mawili ya Maswa ambapo katika jimbo la Maswa Magharibi kiasi cha shilingi bilioni 1.014,200,200/= zimetumika kujenga shule mbili mpya za msingi na madarasa ya mfano ya chekechea ambapo shule moja ni ya mikondo miwili iliyopo Kijiji cha Jija Kata ya Jija,ujenzi wa shule mpya ya msingi Majengo yenye mkondo mmoja iliyopo Kijiji cha Shishiyu kata ya Shishiyu ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa na matundu ya vyoo 3 katika shule ya msingi Igunya iliyopo Kata ya Jija pamoja na ujenzi wa madarasa ya mfano ya chekechea katika shule ya msingi Mwabayanda Kata ya Mwabayanda.
Kwa upande wa Maswa Mashariki kiasi cha shilingi milioni 567,400,000/= zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Mwakabeya yenye mkondo mmoja, ujenzi wa vyumba vya madarasa 3 na matundu matatu ya vyoo katika shule ya msingi Ipililo B, ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu na matundu ya vyoo katika shule ya msingi Ngudu iliyopo Kata ya Bugarama, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu 3 ya vyoo katika shule ya msingi Nguliguli iliyopo Kata ya Nguliguli.
“Fedha hizi zote shilingi bilioni 1,581,600,000/= zimepelekwa kuboresha miundombinu mbalimbali na ujenzi wa shule mpya kabisa za kisasa ambappo kwa mazingira hayo imeweza kupunguza adha kubwa ya msongamano wa wanafunzi katika maeneo mbalimbali, imeboresha miundombinu kwa hiyo mazingira ya ufundishaji kwa sasa yamekuwa bora kabisa na changamoto zote za ufundishaji zitakuwa zimeisha” Alisema Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa upande wa walimu wakuu waliopata fursa ya mradi huo wamemshukuru Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha hizo za ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu kwa sababu ametatua changamoto katika shule hizo ambazo wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta elimu, pia kulikuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi katika darasa moja hivyo ujio wa shule hizo utaboresha mazingira ya ufundishaji na watoto wa chekechea wataweza kusoma vizuri na kwa kuzingatia umri wa kuanza masomo hayo.
Nao watendaji wa Kata wamemshukuru Mhe Samia Suluhu Hassan kwa miradi hiyo ambayo itasaidia wanafunzi kutatua kero mbalimbali za wanafunzi kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi katika darasa moja sambamba na hilo wamemuahidi Mhe Rais kuwa miradi hiyo watailinda na kuisimamia vizuri ili idumu kwa muda mrefu.
Wanafunzi wa shule mbalimbali zilizonufaika na mradi huo wamemshukuru Mhe Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea miundombinu hiyo ya madarasa, vyoo na shule hizo mpya ambapo itasaidia kutatua changamoto ya kukaa dawati moja wanafunzi watano au wanne, pia wamesema vyoo hivyo vitasaidia kuokoa muda wa masomo maana kabla ya mradi huo vyoo vilikuwa vichache hivyo kupoteza muda mwingi wa masomo na wameahidi kusoma kwa bidii ili wawe viongozi wakubwa wa baadae katika taifa hili.
Kwa nyakati tofauti wananchi nao hawakuwa nyuma kumpa kongole Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa miradi hiyo kwa sababu wananchi hawajachangia fedha yoyote wala nguvu kazi katika miradi hiyo na pia wameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kuwaona na kupeleka miradi hiyo katika maeneo yao ambapo kwa kiasi kikubwa itasaidia Watoto wao kusoma katika mazingira mazuri.
Majengo ya vyumba vya madarasa katika Shule Mpya ya Msingi Majengo iliyoko Shishiyu
Majengo ya vyumba vya Madarasa katika Shule ya Msingi Mwakabeya
Muonekano wa madarasa ya Awali katika Shule ya Mwabayanda
Muonekano wa Shule ya Awali ya Majengo iliyoko Shishiyu
Vyumba 2 vya Madarasa katika Shule ya Msingi Igunya
Vyumba 2 vya Madarasa katika Shule ya Msingi Nguliguli
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.