Mwenge wa uhuru Wilayani Maswa umepokelewa kwa furaha nderemo na vifijo katika kijiji cha Jihu Kata ya Badi ukitokea Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Ulikabidhiwa Wilayani Maswa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuupokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na baadaye kumkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Maswa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali pamoja na timu yake wameridhia miradi yote mwenge uliyopitia kama ilivyopendekezwa na uongozi wa Wilaya ya Maswa. Aidha Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa amefurahishwa na juhudi za wananchi kubuni miradi na hatimaye Serikali kuunga nguvu zao.
Mwenge wa Uhuru Wilayani Maswa umeweka jiwe la Msingi katika mradi wa Maji Jihu - Ikungu na kupanda miti katika eneo la chanzo cha maji hayo katika kijiji cha Nyashimba, Umetoa hati kwa Wananchi wa Mji wa Malampaka ikiwa ni hatua ya urasimishaji ardhi kwa Wananchi, Umeweka Jiwe la Msingi katika Kiwanda cha kusindika Viazi Lishe kilichopo Njiapanda Kata ya Isanga, Umetembelea, kuona na kukagua mradi wa barabara ya Lami yenye urefu wa Km. 1.5 mjini Maswa na umefungua Vyumba 2 vya Madarasa na ofisi 1 katika Shule ya Sekondari Sukuma.
Kiongozi wa mbio za Mwenge amekagua mabanda mbali mbali ambayo ni banda la TAKUKURU ambapo amezindua Klabu ya kupambana na rushwa ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lalago, Banda la mapambano dhidi ya madawa ya Kulevya chini ya Klabu ya Wapinga madawa ya kulevya kutoka katika shule ya Sekondari Lalago, banda la uchaguzi lililokuwa linatoa elimu ya uchaguzi hasa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, banda la wajasiliamali mbali mbali (vikundi vya Vijana, akina Mama na Walemavu) wakiwa na bidhaa zao na banda la afya ambapo amegawa vyandarua kwa akina Mama wajawazito, Watu wenye ulemavu na akina Mama wenye watoto chini ya miaka 5. Aidha baada ya kukagua mabanda hayo alikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi 6,800,000/= kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu.
Wananchi Wilayani Maswa wamejitokeza kwa wingi katika vijiji vyote Mwenge ulipopita huku wakishangilia katika makundi mbalimbali.
Baada ya kazi zote hizo shamrashamra ziko Lalago kisha kesho utakabidhiwa katika kijiji cha Sangaitinje Wilaya ya Meatu.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni Haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.