Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge ameishukuru Serikali kwa kutoa Fedha kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa ajili ya uboreshaji usalama wa milki za ardhi ili kutekeleza mpango wa matumizi ya ardhi, kuandaa matumizi sahihi ya vijiji kupitia mipaka mipya na kutoa hati miliki za kimila katika wilaya ya Maswa.
Mradi huo umepanga kuboresha usalama wa milki ya ardhi kwa kupanga, kupima, kusajili hati milki za kimila laki tano(500,000) ambapo wilaya ya Maswa inakusudiwa kunufaika na mradi huo kwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ya vijiji 100 na kuandaa hati milki za kimila 100,000.
Mkuu wa Wilaya amesema hayo katika kikao Cha wadau katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wakati wadau wakijadili mpango wa matumizi ya ardhi wilaya ya Maswa.
Mpango wa matumizi ya ardhi ya Wilaya umeainisha miradi mbalimbali inayopaswa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 20 ijayo ili kutatua changamoto zilizoainishwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Maswa.
Mhe. Kaminyoge amesema kutokana na ongezeko la watu mji umebadilika kuwa na migogoro ya ardhi, ukuaji wa makazi yasiyopangwa, upungufu wa huduma za jamii na uharibifu wa Mazingira ili kukabiliana na changamoto hizo wilaya haina budi kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ambayo ni nyenzo ya upangaji inayoainisha matumizi mbalimbali ya rasilimali ardhi kulingana na hali halisi ya kiuchumi na kijamii.
Aidha mkuu wa Wilaya amesema utekelezaji wa mpango huo katika Halmashauri ya Maswa utaleta matokeo chanya katika kuchochea maendeleo ya Wilaya pamoja na kuleta usalama wa milki za ardhi, kukuza huduma za kijamii, kuboresha uhifadhi wa Mazingira na kumaliza migogoro inayotokana na ardhi.
"Naamini mpango huu ni mwarobaini wa matatizo ambayo waheshimiwa madiwani, waheshimiwa wabunge, Mkurugenzi Mtendaji, watendaji wa Kata na vijiji mnapambana nayo katika shughuli za kuwahudumia wananchi." Amesema Mkuu wa wilaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Maisha Mtipa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta mradi huo wa uboreshaji wa usalama mradi ambao unaenda kutatua kero za mipaka, na migogoro ya matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake meneja mradi wa urasimishaji vijijini Bw Joseph Onesmo amesema serikali imetoa Fedha kiasi Cha shilingi US Dola milioni 150 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 345 kutekeleza mradi huo katika wilaya Saba za Tanzania ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imepata kiasi Cha shilingi bilioni 3 kutekeleza mradi huo.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe. Paul Maige amemshukuru Rais kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa fursa waliyoipata ya mradi huo mkubwa ambao unatekelezwa katika Halmashauri Saba tu Tanzania nzima, pia amewaomba kila mmoja akasimamie na kushiriki kikamilifu katika mradi huo ili kuhakikisha Halmashauri inazalisha kwa tija ili kuinua uchumi na kuchangia kwa asilimia kubwa katika ajira.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.