Shirika la kiserikali linalohusika na tafiti mbalimbali za wadudu waharibifu la Tropical Pesticides Research Institute (TPRI) limefanya mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa Kilimo na baadhi ya wanachama kutoka katika AMCOS za Wilayani Maswa chini ya ufadhili wa washikadau GATSBY AFRICA.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia tarehe 20 - 22/11/2019 kwa nadhalia na vitendo. Malengo makuu ya mafunzo hayo yalikuwa yafuatayo:-
1.Kufundisha sheria na kanuni ya udhibiti wa visumbufu vya mimea Tanzania
Madhumuni ya sheria na kanuni ni
•Kulinda afya ya binadamu, wanyama na viumbe wengine rafiki wa mazingira
•Kuongeza ubora wa mazao kulingana na mahitaji ya masoko
•Kuelekeza matumizi sahihi ya viuatilifu ili kuongeza mavuno kwa mazao ya chakula na biashara
2.Kufundisha visumbufu mbalimbali vya zao la pamba na njia za kudhibiti
3.Kufundisha madhara ya viuatilifu na huduma ya kwanza.
4.Kufundisha vibandiko na vielekezo vya michoro
5.Kufundisha vifaa kinga vya kuzuia viuatilifu visiingie mwilini
6.Kufundisha matumizi sahihi ya vinyunyizi (Mabomba) na vinyunyizio(Nozeli) vya kunyunyizia viuatilifu.
7.Kufundisha mbinu bora za unyunyiziaji wa viuatilifu
8.Kufundisha uhifadhi sahihi na uteketezaji wa viuatilifu chakavu na viwekeo tupu.
Siku ya kwanza walielekezwa mambo mbalimbali ikiwemo utambuzi wa visumbufu ( wadudu, magonjwa, magugu), njia za udhibiti wa visumbufu vya zao la pamba, aina na tabia ya viuatilifu na michanganyiko ya viuatilifu.
Siku iliyofuata baada ya wajumbe kufundishwa vibandiko, vielelezo vya michoro, vifaa kinga vya kuzuia viuatilifu visiingie mwilini pamoja na mbinu bora za unyunyiziaji wa viuatilifu, walienda shambani kwa ajili ya kutambua aina ya visumbufu ili kuelewa ni aina gani ya kinyunyizio (nozeli ) watumie wakati wa kunyunyizia kulingana na visumbufu vilivyopo shambani Mfano; wadudu, magonjwa au magugu.
Siku ya mwisho walielekezwa jinsi ya kufanya maandalizi ya mabomba kabla ya kunyunyizia viuatilifu, hii ni pamoja na uchanganyaji sahihi wa viuatilifu hivyo. Pia walijifunza mbinu bora za unyunyiziaji viuadudu,vizuia kuvu na viuagugu.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.