Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Usimamizi Ufatiliaji na Ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkoa wa Simiyu Ndg. Pius Ngaiza amewataka Waheshimiwa Madiwani kusimamia ukusanyaji wa mapato kikamilifu kwa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato vya kisasa na kuachana na vyanzo vidogovidogo ambavyo vinakuwa kero kwa wananchi, na kusimamia maagizo mbalimbali yanayotolewa na serikali ili yatekelezwe kwa wakati.
Pia ameongeza kuwa Waheshimiwa Madiwani kusimamia ukamilishaji wa miradi ambayo ipo kwa muda mrefu kwa kuongeza kasi katika ukamilishaji wa miradi hiyo kwa kushirikiana na wanachi katika miradi ambayo wananchi wameianzisha ili kuondoa ugumu wa wananchi kuchangia nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Ameongeza kuwa Waheshimiwa Madiwani wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa viongozi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI watakaokuja katika maeneo yao kwa ajili ya kuhakiki maeneo ya Utawala ili kuandaa utekelezaji wa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika 2024 hivyo amewataka madiwani kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi hao.
Amezungumza hayo katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa Fedha 2022/2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Leo tarehe 07/09/2023 wakati wa uwasilishaji wa taarifa za kata katika kipindi cha robo ya nne ya baraza la madiwani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mr. Maisha Mtipa ametoa wito kwa watendaji wote wa Kata kuboresha taarifa zao zinazohusiana na masuala ya mapato, miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata zao ili kuleta ushindani katika kila robo ya mwaka ili kuona ufanisi na utendaji kazi wa viongozi hao katika maeneo yao.
Pia Mr Mtipa amesisitiza kuwa katika hali ya chakula ajenda ya afua za lishe iwe ni muhimu katika miezi 3 kwa kufuatilia hali ya utoaji wa chakula katika shule unaendeleaje na ni shule ngapi zinatoa chakula katika Kata hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe Paul Maige amewapongeza watendaji wa Kata kwa usimamizi mzuri wa mapato ya Halmashauri katika maeneo yao kwa kuwa yameimalika.
"Watendaji wa Kata Wana nafasi kubwa sana ya kutufanya tufanikiwe kwa kufikia malengo tuliyojiwekea mkizembea tu maana yake ni kwamba mmeiangusha timu ya menejimenti, mmeliangusha baraza la madiwani kwa maana ya menejimenti na waheshimiwa madiwani nyie ndio mmeshika mpini kwa hiyo Simameni imara kwa yale mazuri mliyoyafanya kama kuna sehemu ambayo hamkufanya vizuri basi hakikisheni mianya hiyo mnaiziba ili tuweze kufanikiwa tunapojiwekea malengo tunahitaji tuyafanye."amesema Mhe. Maige.
Kwa upande wao Waheshimiwa Madiwani wamempongeza Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo miundombinu ya afya, barabara, Elimu, maji inayotekelezwa katika Kata zao na wameahidi kuendelea kumuunga mkono katika masuala yote ya maendeleo katika maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.