Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa Ndg Athuman Kalage amesema kikao hicho kimeitishwa lengo likiwa ni kuwawezesha waheshimiwa madiwani kupata Elimu kuhusu masuala ya kisheria na kanuni za kilimo bora cha pamba kwa kuwa wao ndio wanakaa na wananchi kwa karibu.
Ameongeza kuwa kikao hicho kilikuwa mahususi kwa ajili ya waheshimiwa madiwani ili kuwe na uelewa wa pamoja katika kutekeleza masuala ya Kilimo cha pamba ambacho kitasaidia kuongeza ubora zaidi kuliko sasa.
Aliyasema hayo katika mafunzo ya Kilimo Bora cha zao la pamba kwa waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambapo kikao hicho kilihusisha wakuu wa Divisheni, Kamati ya ulinzi na usalama na wadau wengine wa masuala ya pamba, balozi wa pamba Tanzania pamoja na viongozi kutoka bodi ya pamba Tanzania.
Mkaguzi wa pamba kutoka bodi ya pamba Tanzania Mr Daniel Bariyanka alisema bodi ya pamba Tanzania imepanga kuanzisha mashamba darasa katika kila Kitongoji kilichopo katika Kijiji husika lengo ni kuwawezesha wananchi kujifunza kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba kabla ya msimu kuanza ili wakienda kulima waweze kufuata hatua zote zinazostahili ikiwepo kipimo cha sentimita 60 kwa 30 ili walime kwa tija na kupata mavuno mengi.
"Vile vipando sasa tunavitoa Nyakabindi tunataka tuvipeleke katika kila Kitongoji kinachopatikana katika kila Kijiji kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, kama Kijiji kitakuwa na vitongoji 5 kila Kitongoji kitakuwa na kipando kutokana na idadi ya vitongoji vilivyopo katika Kijiji husika". alisema Mr. Bariyanka
Kwa upande wake balozi wa pamba Tanzania Mhe Agrrey Mwanri amewataka madiwani kutoa muda wao kwa kuhamasisha wananchi kuhusu Kilimo Bora cha zao hilo kwa kulipa umuhimu suala hili kwa kuwa waheshimiwa madiwani wamebeba nafasi kubwa katika jamii hivyo wanawajibu wa kusimamia kikamilifu ili wananchi wao waongeze tija na uzalishaji katika zao hilo.
Mashamba darasa hayo yatawekwa katika maeneo ya wazi ambayo yatafikiwa na kila mtu kwa ajili ya kupata ujuzi wa mbinu bora za kilimo cha pamba maeneo hayo yatakoyotumika katika kuanzisha vipando hivyo yatakuwa ni maeneo ya msikitini, kanisani, barabarani, maeneo ya senta, mashuleni, madukani, mashineni ambapo watu wengi wanapita lengo ni kila mkulima aone kwa macho vipimo vya sentimita 60 kwa 30 vinatumikaje shambani.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa Ndg. Makota amewaomba waheshimiwa madiwani na viongozi kufuata maelekezo ambayo yametolewa kwenye semina hiyo yakifanyika mara kwa mara wakulima watabadili mtazamo wa kuweka tija kwenye zao la pamba pamoja na hilo amewaomba waheshimiwa madiwani elimu waliyoipata wakaitumie vizuri kuwahamasisha wananchi wakaone tija inayopatikana baada ya kufuata sheria na kanuni za kilimo hicho.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe Paul Maige amemshukuru balozi wa pamba kwa ushauri aliotoa kwa kuwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ndio msingi wa mambo yote hayo ya kuongeza uzalishaji kwa kutoka kwenye vipimo vya sentimita 90 kwa 40 kwenda kwenye vipimo vya sentimita 60 kwa 30 ambayo itakuwa imekidhi viwango na kuongeza tija kwa wakulima.
Nae mkuu wa Divisheni ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Ndg. Robert Urassa alisema katika msimu wa 2023/2024 Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa inatarajia kulima heka 60,438 za pamba na kutalajia kuzalishaji zao hilo kwa wastani wa kg 400 kwa ekari ambapo inatakiwa kuzalisha Tani 60,438.
Pia Mr Urassa ameongeza kuwa mikakati mbalimbali imewekwa ikiwepo kuhamasisha wakulima na viongozi wote juu ya uongezaji tija kwa kufuata kanuni za Kilimo bora cha pamba, kusimamia upatikanaji na ugawaji wa pembejeo za pamba kwa wakati ili kuwasaidia wakulima kulima mapema zao hilo.
Kwa upande wake mkaguzi wa pamba Wilaya ya Maswa Mr Ally Mabrouk alisisitiza ushirikiano kwa viongozi wote katika kuhamasisha wananchi kufuata kanuni 10 za Kilimo cha pamba ambacho kinaanzia hatua ya usafishaji wa mashamba mpaka namna bora ya kuvuna pamba ili kuwasaidia wananchi kupata mavuno mengi katika zao hilo.
Pia ameongeza kuwa wananchi wakitumia kanuni hizo za Kilimo cha pamba watanufaika katika uzalishaji kwa kuongeza tija katika zao hilo ambalo litawaongezea kipato na kuwaletea maendeleo katika uchumi wao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.