Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu Mhe Aswege Kaminyoge amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa kwa watoto waliopata ujauzito kupata elimu kama wanafunzi wengine lengo likiwa ni kuwasaidia watoto wa kike kuendelea na masomo ili watimize ndoto zao.
"Nimpongeze kwa kile alichokieleza kwamba watoto wa kike ambao wanakosa Elimu kwa kupata ujauzito wakishajifungua warudi darasani ili waendelee na utaratibu wa kupata Elimu kama wanafunzi wengine" Amesema Mhe Kaminyoge.
Amesema hayo wakati wa maadhimisho ya wiki ya Elimu ya watu wazima yaliyofanyika katika uwanja wa nguzo nane wilayani Maswa leo tarehe 25.09.2023 wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Dkt Yahaya Nawanda ambapo maadhimisho hayo yamefanyika Kimkoa wilayani Maswa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa, wakuu wa Wilaya za Simiyu, wakurugenzi wa Halmashauri, makatibu Tawala wa Wilaya, maafisa Elimu wakuu wa Divisheni na vitengo walimu pamoja na wanafunzi.
Pia ametoa wito kwa wananchi wote kuwaruhusu wasichana wote waliokatisha masomo wenye sifa za kurudi shule waweze kurejea shuleni na kuendelea na masomo na sambamba na hilo amewataka makatibu tawala wa wilaya zote kuchukua hatua za kisheria kwa watoto wote wanaopata ujauzito ili watoto hao baada ya kujifugua waweze kuendelea na masomo.
Mhe kaminyoge amewasisitiza wakurugenzi wote kuanzisha madarasa ya kisomo ambayo yatakuwa endelevu ili kukabiliana na tatizo la stadi za kujifunzia yaani kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) pamoja na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuendesha elimu ya watu wazima.
Aidha amewataka walimu wote waliohitimu stashahada ya elimu ya watu wazima kufundisha na kusimamia elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi katika vituo vyote na shule zenye mahitaji maalumu.
Nae Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu Ndg Majuto Nganja amesema maadhimisho hayo yanalenga kutathmini shughuli za elimu ya watu wazima inavyoendeshwa katika Mkoa wa Simiyu kwa kupata taarifa za utekelezaji wa shughuli za elimu ya watu wazima kwa kuonyesha shughuli mbalimbali zinazofanyika katika elimu hiyo.
Aidha ameongeza kuwa serikali kupitia mpango wa elimu ya sekondari ulitoa fursa kwa wanafunzi wote walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwepo ujauzito na mazingira magumu waweza kujiunga na vituo vya elimu ya watu wazima vilivyopo katika Mkoa wa Simiyu.
Pia amesisitiza kuwa wananchi wote ambao walikosa kusoma kwenye mfumo rasmi wanatakiwa kujiunga katika vituo ambavyo vipo katika kila shule ya sekondari na shule ya msingi ili waweze kupata uelewa wa kujua kusoma na Kuandika fursa ambayo italeta maendeleo kwa jamii na nchi nzima kwa ujumla.
Kwa upande wao wasichana wanaosoma katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malampaka ambao walipata ujauzito wakati wakisoma wamemshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fursa ya kusoma tena ili waweza kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake Afisa Elimu ya watu wazima, Elimu nje ya mfumo usio rasmi na Elimu maalumu Mkoa wa Simiyu Ndg Esta Warwa amesema katika Mkoa wa Simiyu vituo 8 vya Elimu mbadala vimeanzishwa kwa ajili ya wasichana waliokatiza masomo ambapo mpaka sasa wasichana 222 wamerudi shuleni kuendelea na masomo na vituo hivyo vipo katika wilaya zote za Simiyu.
Maadhimisho ya juma la Elimu ya watu wazima yamefanyika kwa mgeni rasmi kutembelea mabanda mbalimbali kutoka katika vyuo vya VETA, Vikundi mbalimbali na Banda la stadi za kujifunzia. Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya "Kukuza uwezo wa Kusoma na Kuandika kwa Ulimwengu Unaobadilika: Kujenga Misingi ya Jamii Endelevu na yenye Amani".
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.