Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani Maswa ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hii Mhe. Dr. Seif Shekalage imetembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa ikiwemo na miradi ya kimkakati. Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni kama ifutavyo:-
Ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa
Katika mradi huu wanakarabati Mabweni, Madarasa, Nyumba 17 za Walimu, Zahanati, Bwalo na Ofisi. Ukarabati huo uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo baadhi ya majengo yameishakamilika. Katika ukaguzi huo Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha shughuli hiyo katika maeneo yote aliyopita na kukagua.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani Maswa ikikagua Bweli lililokamilika ukarabati wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo
Mkuu wa Wilaya ya Maswa akitoa maelekezo kuhusu ukarabati sehemu ya jiko
Mradi wa Maji Nguliguli
Mradi huu unatarajia kuhudumia vijiji viwili. Katika kijiji cha Nguliguli litajengwa Tenki lenye ujazo wa lita 100,000, Vituo 12 vya kuchotea maji na nywesheo la mifugo 1. Kijiji cha Mwamanenge litajengwa Tenki lenye ujazo wa lita 90,000, Vituo 9 vya kuchotea maji na nywesheo la mifugo 1.
Mkuu wa Wilaya ameagiza Mkandarasi afike eneo la kazi na kuanza utekelezaji wa ujenzi mapema. Aidha ameagiza mkandarasi awasilishe mpango kazi wake wa kutekeleza shughuli hii ofisini kwa mkuu wa Wilaya siku ya Ijumaa.
Miradi ya kimkakati
Inahusisha ujenzi wa Kiwanda cha Chaki na Kiwanda cha Vifungashio katika kijiji cha Ng'hami. Kakita miradi hii Mkuu wa Wilaya ameagiza taratibu za vifaa vya ujenzi zikamilike haraka na kazi ya ujenzi iendelee.
Ujenzi Ofisi ya Udhibiti Ubora
Ujenzi wa ofisi hii umekamilika, fundi ameahidi kukabidhi jengo kesho, huku samani akisema atakabidhi siku ya Jumapili ya tarehe 24/11/2019.
Kutokana na salio lililobaki Mkuu wa Wilaya ameelekeza wajenge uzio.
Ujenzi wa Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Wilaya Maswa
Ujenzi huu uko katika hatua ya ukamilishaji, kazi zilizobaki ni kuweka Vigae, Skiming, Milango na Madirisha. Mkandarasi ameahidi kukabidhi jengo hilo tarehe 15/12/2019.
Mradi wa Maji Mhida
Ujenzi wa Tenki unaendelea na kuweka mtandao wa bomba.
Mkuu wa Wilaya amemuagiza Meneja RUWASA kupeleka mpango kazi wa utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa ujenzi Chuo cha Maendeleo Malampaka
Mradi huu unahusisha ujenzi wa Mabweni 2 na Bwalo, Ukarabati wa vyumba 4 vya madarasa, vyoo, karakana ya ushonaji, maabara ya ICT, Kuchimba kisima na uwekaji wa mfumo wa maji na umeme.
Mhandisi kutoka Wizara ya Elimu baada ya kufanya ukaguzi wa Mradi amesifu jitihada zinazoendelea kwa kazi nzuri na iko hatua nzuri na ameahidi kuongeza nguvu kwenye ukarabati wa Jengo la Utawala.
Aidha kupitia maongezi kati ya Mtaalamu wa Wizarani na Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ameshukuru kwa utaratibu huo wa Wizara kufika kuona maendeleo ya Miradi yao na kuiomba kuongeza muda zaidi ili kupitia miradi yote.
Kwa msisitizo Mkuu wa Wilaya amewaambia Wahandisi wahakikishe wanafika kukagua na kutoa maelekezo ya kitaalamu kila wiki kwenye miradi hii inayoendelea ili kuwa na majengo bora japo wa majengo mengi ya kusimamia.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Mwabayanda
Kazi ya Ujenzi wa Jengo la Wodi ya Wazazi, Upasuaji, Maabara, kuhifadhi maiti na nyumba ya Mtumishi uko katika hatua ya ukamilishaji. Viongozi wamesema imefika muda sasa ujenzi huu ukamilike na majengo yaanze kufanya kazi. Mhandisi amesema Mwezi ujao yatakuwa tayari ya mekamilika.
Shule ya Msingi Mwandu
Katika shule hii vyumba 3 vya madarasa na ofisi viliezuliwa na upepo siku ya tarehe 17/11/2019
Mkuu wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi kuhakikisha ukarabati unafanyika haraka ili kunusuru vifaa vilivyobaki salama na kuweka mazingira ya utayari kwa ajili ya Wanafunzi kuendelea na masomo katika mazingira mazuri ya kujifunzia.
Mkuu wa Wilaya akitoa maelekezo ya kukarabati Jengo lililoezuliwa na upepo katika shule ya Msingi Mwandu
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.