Kamati ya kudumu ya mikopo ngazi ya Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imepata mafunzo maalumu kwa ajili ya usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo yametolewa kwa kamati hiyo ambayo inaundwa na Mtendaji wa Kata, Afisa Maendeleo ya jamii, Afisa Ustawi wa Jamii, Afisa Elimu Kata, Maafisa Ugani na Mifugo wa Kata, Watendaji wa Vijiji pamoja na Polisi Kata ili kufahamu kanuni taratibu na miongozo ya utoaji wa mikopo .
Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 23 oktoba 2024 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Awali Serikali ilisitisha utoaji wa fedha za mikopo kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kuanzia April hadi Juni, 2023 ili ijipange vizuri kuweka mfumo mpya wa utoaji wa mikopo.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndugu Vivian Christian amesema serikali imekuja na mpango kazi ambao kila mtu atashirikishwa kwenye ngazi ya eneo husika ili kusimamia kikamilifu utaratibu mzima wa mikopo ya asilimia 10.
Serikali imerejesha rasmi utaratibu wa mikopo isiyo na riba ambayo ilikuwa ikitolewa kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.
Pia amesema mafunzo kama hayo tayari yametolewa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Mikopo ya Halmashauri ya Wilaya.
Aidha ametoa wito kwa washiriki hao kuhakikisha wanasikiliza kwa makini mafunzo hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri kwa kuwa wao ndio watahusika kusaidia nyaraka mbalimbali za wanavikundi ambao wanaishi nao katika maeneo yao.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya Jamii Lusia Misinzo amesema serikali imeweka utaratibu mzuri ambao umepanua wigo kwa makundi maalum ambapo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wenye umri wa miaka 18- 45 wanaweza kukopa tofauti na awali ambapo serikali iliruhusu umri usiozidi miaka 35 sambamba na hilo pia mtu binafsi anaweza kukopa lakini lazima awe kwenye kikundi.
Kamati hiyo itakuwa na majukumu ya kupokea na kuchambua maombi ya mikopo, kufanya tathmini ya awali ya maombi yaliyowasilishwa kwa kutembelea kuhakiki na kushauri vikundi vilivyoomba mikopo na kuandaa taarifa ya hali halisi ya vikundi hivyo na kuwasilisha katika kamati ya mikopo ya Halmashauri.
Aidha kamati hiyo itajikita kwenye ufuatiliaji wa marejesho, kuona maendeleo ya shughuli zao, kushirikisha wadau kutoa mafunzo kwa vikundi na kuwasilisha taarifa ya mikopo kwa kamati ya maendeleo ya Kata.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.