Kamati ya Bunge, Maliasili na Utalii imefanya ziara katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu yenye lengo la kukagua mradi wa matumizi bora ya milki za ardhi ambao kamati imeridhishwa na mradi huo ambao una faida kubwa ya kusaidia kupunguza migogoro mingi ya ardhi katika mipaka ya vijiji, mashamba na kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya ardhi, maliasili na utalii Mhe Timotheo Mzava katika nyakati tofauti walipotembelea na kukagua mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi katika vijiji viwili, Kijiji cha Mwadila kilichopo Kata ya Sukuma na Kijiji cha Igongwa kilichopo Kata ya Ng'wigwa walipokuwa wakigawa hati za kimila 50 kwa kila Kijiji.
"Maelezo tuliyoyapata, maelezo mliyoyatoa nyinyi wenyewe na ramani tuliyoelekezwa sisi kama kamati tumeridhika, kazi hii inafanyika vizuri, tumekuja kuona ni kweli serikali na Wizara wamefanya kazi hiyo vizuri." Amesema Mwenyekiti wa kamati.
Aidha Mhe Mwenyekiti wa kamati amewapongeza wananchi kwa kuupokea mradi huo kwa kuwa utakwenda kuongeza thamani katika ardhi yao na kupitia mradi huo Maisha yao yataboreka.
"Mradi huu ni mradi mkubwa sana unakwenda kuongeza thamani sana lakini kama hauna uthibitisho wa umiliki wa ardhi hiyo wakati mwingine thamani yake inakuwa sio nzuri sana kwa kazi nzuri hii iliyofanywa na Wizara, nataka niwahakikishie kuwa ardhi yenu inaenda kuongeza thamani ". Amesema Mhe Mzava
Pia Mhe Mzava amewasisitiza viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia maeneo yote yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali hayaigiliwi kutokana na makubaliano yaliyo katika mpango huo kwa kuwa serikali imewekeza Fedha nyingi katika mradi huo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Mbunge Geofrey Pinda amesema mradi huo una lengo la kufanya maboresho katika vijiji ili kuwe na matumizi bora ya ardhi ambapo mradi huo unatekelezwa katika wilaya saba Tanzania nzima na Maswa ni miongoni mwa Wilaya inayonufaika na mradi huo.
Ameongeza kuwa vijiji 106 vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ambapo vijiji 5 vitaingia Halmashauri ya mji wa Maswa kwa ajili ya upanuzi wa mji na vijiji 9 vitapata hadhi ya kuwa miji midogo lengo ni kubeba vijiji vingine ili vikue.
Mpango huo pia utawafaidisha wananchi kwa kuwa hekta 77,666 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji, hekta 481 kwa ajili ya taasisi mbalimbali na hekta 713 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
"Nawaomba wananchi kujitokeza kuhakiki majina yenu ukipata kile kipande cha karatasi unayo haki ya kwenda benki nyie wakulima mnahitaji mikopo masharti yanakuwa mengi lakini ukiwa na hati hii tayari unaweza ukaigia benki na ukaaminiwa ukapewa mkopo kwa sababu wanajua watakukuta wapi." Amesema Naibu Waziri
Nae Afisa Ardhi Wilaya ya Maswa Ndg Vivian Christian amesema mradi huo utasaidia kuthibiti uvamizi katika maeneo yote ya umma yaliyopo katika vijiji hivyo pamoja na kuongeza usalama,ufanisi na suluhisho la utatuzi wa migogoro kwa wananchi.
Aidha ameongeza kuwa mpaka sasa mradi huo umegharimu shilingi milioni 819 ambapo vijiji 32 vimeandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi na vipande vya ardhi 19,885 kutoka vijiji 14 vimepimwa na kuingizwa kwenye mfumo na mradi huo utakuwa suluhisho la kuongeza usalama, ufanisi na utatuzi wa migogoro.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.