Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu Mhe. Aswege Kaminyoge amekagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Maswa na kuwaomba wataalamu kusimamia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Akiwa katika ziara hiyo iliyofanyika leo tarehe 22 februari 2023 ya kukagua miradi Mhe. Mkuu wa Wilaya aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Maswa, wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Mhe. Kaminyoge amekagua ujenzi wa zahanati ya Nguliguli iliyopo Kata ya Nguliguli unaohusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), Jengo la Cliniki (RHC) na ujenzi wa nyumba moja ya mtumishi na ujenzi wa vyoo ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya ukamilishaji.
Mradi huo wa ujenzi wa zahanati hiyo unatekelezwa kwa fedha za Global Fund ambapo kiasi cha shs 271,096,536/= kimetolewa katika mradi huo na mpaka sasa mradi huo umetumia shs 144,610,043.98/=, ujenzi wa shule mpya msingi Mwabaraturu iliyopo kata ya Mpindo inayohusisha vyumba 9 vya madarasa, jengo la utawala 1 na matundu ya vyoo 30 katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Mradi huo wa ujenzi wa shule hiyo unatekelezwa na serikli kuu ambapo shs 250,000,000/= zimetolewa kutekeleza mradi huo na shilingi milioni saba zimetolewa na mfuko wa jimbo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili yaliyojengwa na wananchi. Pia ametembelea ujenzi wa jengo la kufulia nguo katika Kituo cha Afya Zebeya.
Pia Mhe Mkuu wa Wilaya alitembelea shule ya sekondari Ipililo, kituo cha afya Ipililo pamoja na bwawa la Zebeya kuona huduma zinavyotolewa katika maeneo hayo.
Mhe kaminyoge amesema serikali imetoa fedha ili kuboresha sekta ya elimu na afya hivyo amewasisitiza mafundi wote kuhakikisha wanajenga kwa viwango ili majengo hayo yaweze kudumu kwa muda mrefu na kukamilika kwa muda uliopangwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.