Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge ametoa shukrani kwa Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha miundombinu ya elimu na ufundishaji na ujifunzaji inaboreshwa kwa kutoa vifaa vya tehama vyenye lengo la kuwezesha mafunzo endelevu ya walimu kazini.
Mhe kaminyoge ametoa kauli hiyo wakati akikabidhi vifaa vya Tehama kwa maafisa elimu kata, walimu wakuu vilivyotolewa na serikali kupitia mradi wa BOOST ambapo ametoa wito kwa walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weredi na uadilifu mkubwa kwa kuwa mpaka sasa matokeo ya elimu msingi na sekondari yamepanda.
“ Maafisa elimu kata na wakuu wa shule hivi vifaa vina gharama kubwa maana yake vinatakiwa kutunzwa kama mboni ya macho yenu kwa kushirikiana na afisa elimu, uongozi wa serikali ya kata na vijiji vyenu kuhakikisha mnapata walinzi waaminifu ambao watavilinda na hawatashawishika.” Amesema Mhe. Kaminyoge
Pia Mkuu wa Wilaya amewataka viongozi waliokabidhiwa vifaa hivyo kuhakikisha wanavitunza vizuri na kuviweka kwenye mazingira mazuri yasiyoshawishi kuchukuliwa ili vifaa hivyo vilete tija na kuleta matokeo chanya katika ufaulu.
“Maafisa elimu kata ambao mmepewa jukumu la kuratibu walimu kujifunza kazini hebu pangeni ratiba vizuri ili walimu waweze kupata hayo mafunzo lakini pia afisa elimu ikikupendeza mahali pengine wanapofanya vizuri toa motisha ili na wengine waone.” Mkuu wa Wilaya
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Vivian Christian amesema wamepokea vifaa hivyo kutoka mkoani vikiwa salama na vitapelekwa kwenye vituo vya Malampaka na Binza kwa ajili ya kujifunzia walimu.
Nae Dkt Lucy Kulon’gwa Mkuu wa Divisheni ya elimu ya awali na msingi Halmashauri ya wilaya ya Maswa ametoa pongezi kwa Mhe Rais kwa kuona umuhimu wa kuleta vifaa ambavyo vitakuwa na umuhimu mkubwa katika shule hizo.
Amesema vifaa hivyo vitakaa katika vituo hivyo viwili kwa lengo la kuwawezesha walimu kujifunza na kubadilishana ujuzi katika masomo mbalimbali njia na mbinu za kufundishia ikiwepo mbinu mpya za KKK na pia itasaidia kutumia mitandao ya kijamii kuona namna ambavyo wengine wanavyofundisha ili kurahisisha namna ya ufundishaji.
Aidha Dkt Kulon’gwa ametoa wito kwa walimu kutumia vifaa hivyo na si kuvitunza stoo ili vilete tija kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine ambapo katika kila kituo kinachukua zaidi ya shule 7.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imepokea jumla ya kompyuta mpakato 4, Photocopy Mashine 2, projekta 4, Skrini Na Stendi 4, Smart Tv (Inchi 65) 2, Microphone 2, Zoom Kamera 2, Digital Kamera 2 na Wireless Router 2 ambavyo vimetolewa na serikali kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya vituo viwili vya Binza na Malampaka ambavyo vitawezesha utekelezaji wa mafunzo endelevu ya walimu kazini.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.