Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amesema makampuni yanatakiwa kununua pamba katika AMCOS kwa sababu pamba hiyo inakuwa na ubora unaotakiwa lengo likiwa ni kupunguza kero ya pamba isiyo na ubora.
Amesisitiza kuwa wadau wa pamba ni wakulima, wanunuzi, AMCOS na serikali hivyo amewataka kuongea lugha moja wanapokutana na changamoto, kero na matatizo katika kipindi Cha ununuzi wa pamba.
Mhe. Kaminyoge ameyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa pamba kutathmini zao la pamba katika ununuzi kwa msimu huu wa Kilimo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa leo tarehe 22, Julai 2023
Mhe. Kaminyoge amesema makampuni ya pamba yanatakiwa kutafuta mitaji mikubwa ili kuanzisha viwanda ambavyo vitaongeza thamani kwenye pamba kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kupata soko la uhakika.
Pia amewaomba wadau wa pamba kuendelea kutoa Elimu kwa wakulima kuendelea kuuza pamba yao katika msimu huu pamoja na kuendelea kutoa ufafanuzi kuhusu bei ya pamba kutokupanda kutokana na bei ya soko la Dunia kutokupanda kwa sababu ya nchi nyingi kulima pamba hivyo kusababisha zao hilo lisipande bei msimu huu.
"Bei hiyo ya pamba ni nje ya uwezo wa mkulima, makampuni na ni nje ya uwezo wa serikali, yote haya ni bei ya soko la Dunia, ukilizalisha lazima uliuze na lipate soko likafanye kazi yake, kwa hiyo viongozi mkawaelimishe wakulima waendelee kuuza pamba katika kipindi hiki ambacho serikali inanunua pamba".
Mkuu wa Wilaya amewataka viongozi wa AMCOS kufanya kazi kwa weredi ili kuleta usawa katika makampuni yanayonunua pamba katika Wilaya yote ya Maswa ili msimu unapofungwa kusiwepo na deni lolote kutoka kwa makampuni au mkulima.
Pia Mhe. Kaminyoge ametoa wito kwa watendaji wa vijiji kusimamia kwa karibu makampuni yanayonunua pamba katika maeneo kwa kuwa zao hilo linaingizia mapato ambayo inasaidia kuendesha Halmashauri.
Nao wanunuzi wa pamba wameipongeza Wilaya ya Maswa kwa kuwa pamba inayopatikana ni Safi kwa asilimia kubwa haijachanganywa na maji au mchanga hivyo wamewaomba viongozi wa AMCOS kusimamia vizuri pamba na kutenda haki katika ununuzi wa zao hilo.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.