Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amewataka watendaji wa Kata na wataalamu wa Kilimo kusimamia sheria na kanuni za Kilimo bora cha pamba wanapotoa Elimu hiyo ili wakulima waweze kulima na kuzalisha kwa tija kwa kufuata kanuni zote za Kilimo hicho kwa lengo la kuipatia mapato Halmashauri ili iweze kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema hayo katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya balozi wa pamba katika kampeni ya kuhamasisha wananchi kufuata kanuni za Kilimo Bora na kutolea maelezo kuhusu bei ya pamba kutokupanda kutokana na wakulima wengi duniani kulima zao hilo, ziara ambayo ilifanyika kwa siku sita katika Wilaya ya Maswa.
Mkuu wa Wilaya alisema serikali inatoa pembejeo pamoja na viuatilifu hivyo watendaji na wataalamu wa Kilimo Wanao wajibu wa kusimamia kikamilifu wananchi kwa kutoa Elimu mapema ya kuandaa mashamba yao baada ya msimu kuisha, hii itasaidia kupunguza changamoto ya wakulima wengi kuacha maotea na kuepuka kuchanganya mazao.
Katika hatua nyingine Mhe Kaminyoge ametoa wito kwa Mkuu wa Divisheni ya Kilimo mifugo na uvuvi kufuatilia makampuni binafsi yote yanayonunua pamba yaorodheshwe ili kufahamu utaratibu wanaotumia kununua pamba kwa kuwa kuna baadhi ya makampuni yananunua pamba ambayo haina ubora.
Ameagiza kuwa makampuni yote ambayo yatanunua pamba ambayo haina ubora katika wilaya ya Maswa yatafutiwa kibali na hatua kali zitachukuliwa ikiwepo kupelekwa polisi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Maisha Mtipa amemshukuru balozi wa pamba kwa kutoa elimu kwa nadharia na vitendo ambayo itawasaidia watumishi watakapofika kwa wakulima kutoa elimu vizuri kuhusu kanuni bora za Kilimo Cha pamba.
Pia alisema wamejifunza mambo mengi na wamenufaika nayo ikiwepo ufafanuzi wa bei ya pamba kutokupanda kwa kuwa imewasaidia kwenda kutoa elimu hiyo vizuri endapo watakutana na maswali kutoka kwa wananchi kwa sababu watakuwa na majibu mazuri.
Akitoa taarifa mkuu wa divisheni ya Kilimo, mifugo na uvuvi ndg. Robert Urassa alisema kampeni hiyo imewafikia wananchi 2052 katika vijiji 23 ambao walihudhuria mikutano hiyo ili kupata elimu ya Kilimo Bora cha pamba ambayo imepelekea wananchi 12997 kutoka vijiji 115 kupata elimu hiyo tangu kampeni hiyo ianzishwe mwaka 2021 katika wilaya ya Maswa.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.