Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe Aswege Kaminyoge amefanya ziara katika Kijiji cha Mwashegeshi yenye lengo la kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero na changamoto kwa ajili ya kwenda pamoja katika kutekeleza gurudumu la maendeleo katika Wilaya ya Maswa na taifa kwa ujumla.
Mhe Kaminyoge amesema serikali yoyote duniani imewekwa madarakani na wananchi ili ifanye kazi kwa ajili ya ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi kwa niaba ya wananchi.
Amesema hayo leo tarehe 05.10.2023 katika Kijiji cha Mwashegeshi Kata ya Nguliguli wakati akiongea na wanachi hao kwa kusikiliza kero na kutatua changamoto mbalimbali za maji, afya, Elimu na barabara katika kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya amesema jukumu kubwa la serikali iliyopo madarakani ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani, furaha, utulivu katika kazi zao ili waweze kuzalisha kwa tija katika Kilimo, Mifugo, Biashara pamoja na Uvuvi.
Kwa upande wa maendeleo Mhe Kaminyoge amesema kuwa serikali imetoa Fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miundombinu mbalimbali ya Elimu, Afya, Maji, Kilimo, Mifugo, Barabara na usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 120 vya Wilaya ya Maswa.
Ameongeza kuwa Rais ametoa zaidi ya Shilingi milioni 600 kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji pamoja na ujenzi wa tenki la maji katika Kijiji hicho ili kuwawezesha wananchi hao wanaotunza chanzo cha maji katika bwawa la zanzui kunufaika na maji hayo.
"Ndio maana Mhe Rais amesema katika jambo hili nitalifanya kwa nguvu zangu zote ili wananchi wangu wapate maji, ndio maana katika wilaya ya Maswa Sasa tupo katika asilimia 74% kwa wananchi wa vijijini kupata huduma ya maji ndani ya mita 400. Mhe Rais anasema ifikapo 2025 tufikie 85% , lakini kwa mjini tumefikia asilimia 78% tunataka ikifika 2025 wananchi wapate maji kwa 95% majumbani mwao." Amesema mkuu wa Wilaya
Aidha Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wafugaji kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo maarufu ngitili ili wapate fursa ya mbegu za majani ambayo yatawasaidia ng'ombe wao kuwa na chakula wakati wa kipindi cha uhaba wa nyasi kwa kuwa ng'ombe hao watakuwa na chakula cha kutosha hivyo kuwawezesha wafugaji kufuga kwa tija ili kujiongezea kipato kupitia mifugo.
Kupitia mkutano huo Mhe Kaminyoge amewataka wananchi wote wa Wilaya ya Maswa kuchukua tahadhari katika msimu huu wa mvua ambapo Mamlaka ya Hali ya hewa imetoa utabili kuwa kutakuwa na mvua ya elinino hivyo wanachi wote wanaoishi kwenye mabonde wachukue tahadhari na popote ambapo uharibifu wa miundombinu utatokea wananchi watoe taarifa haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wao wananchi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea miundombinu hiyo ambayo itawasaidia kupata huduma mbalimbali za kijamii sambamba na hilo wamemshukuru Mhe Mkuu wa Wilaya kwa kufika katika kijiji hicho na kusikiliza kero zao na changamoto zao na wameahidi kuendelea kumuunga mkono katika masuala yote ikiwa ni pamoja na kujitolea nguvu kazi kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kijiji chao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.