Afisa lishe wa Mkoa wa Simiyu Bw. Denis Madeleke ametoa wito kwa Divisheni zote kuwekeza katika lishe ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo na udumavu katika mkoa wa Simiyu kwa kuwa matatizo ya lishe hayaondolewi kwa maneno bali yanaondolewa kwa vitendo.
Alizungumza hayo katika kikao cha maandalizi ya mipango na bajeti za afua za lishe kwa mwaka 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na kilichohusisha Kamati ya lishe ya Wilaya pamoja na wakuu wa Divisheni na vitengo.
Afisa lishe alisema katika Mkoa wa Simiyu tafiti zilizofanywa mwaka 2022 zinaonyesha Mkoa wa Simiyu kuna changamoto ya lishe ambapo katika watoto 100 watoto 33% wamedumaa, 68% wanaupungufu wa damu na 50% ya akina mama wana changamoto ya lishe.
“Tukiwekeza katika huduma za mama, tukawekeza katika huduma za vijana tuna uwezo wa kuondoa matatizo ya utapiamlo na njia pekee inayotumika zaidi na inayofanya vizuri ni siku ya afya na lishe ya kijiji tukiweza bukoresha siku ya afya na lishe ya kijiji tunaweza tukaboresha huduma na mwisho wake tukaondoa tatizo la utapiamlo.” Alisema Afisa lishe Mkoa
Aliongeza kuwa ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo mkali vipaumbele vya mkoa ni kuhakikisha huduma hizo Zinatolewa katika Hospitali ya Wilaya pamoja na Vituo vya Afya na Zahanati zote zitatoa matibabu ya kawaida ya utapiamlo pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya kukusanyia taarifa katika jamii.
Pia Bw. Madeleke alisema elimu inatakiwa itolewe zaidi kwa akina mama kuhusu umuhimu wa kutumia chumvi za madini joto kwa sababu itamsaidia mtoto aliyepo tumboni kutengeneza ukuaji wa ubongo wake vizuri pamoja na utoaji wa dawa aina ya FEFO na Foliki Asidi ambayo itawasaidia akina mama kuongeza damu ndani ya miezi mitatu tangu kushika mimba.
Afisa lishe alisisitiza dawa hizo zitasidia akina mama wengi katika mkoa wa simiyu kuepukana na kujifungua watoto wenye vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi, sambamba na hilo elimu ya lishe itolewe vizuri mashuleni ili kusaidia utekelezaji wa afua za lishe.
Kwa upande wake Afisa lishe wa Wilaya ya Maswa Ndg Abel Gyunda alisema Halmashauri imetenga mpango na bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 127 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe katika Divisheni za Halmashauri na vyanzo mbalimbali kwa ajili ya watoto chini ya miaka 5 ili kusaidia kukuabiliana na utapiamlo na udumavu.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dr. Hadija Zegegga alisema ili Wilaya ionekane imefanya vizuri ni lazima fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za lishe zitumike.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.