Zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Maswa limefanyika kwa Amani ambao viongozi mbalimbali wameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi watakao waongoza katika maeneo yao.
Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha Kitongoji cha Mwatonja Kata ya Nyalikungu Mkuuwa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kupiga kura katika vituo 510 vilivyopo katika maeneo yao.
Aidha mhe Kaminyoge amesema kuwa zaidi ya wananchi laki moja na elfu hamsini na tano (155,000) wamejiandikisha kupiga kura hivyo amewataka wananchi wote waliojiandikisha kwenda kupiga kura ili kuchagua viongozi ambao watawaongoza.
“Tunataka wananchi wote waliojiandikisha laki moja na hamsini na tano (155,000) wakapige kura lengo lake na madhumuni yake ni kwamba viongozi watakaochaguliwa wawe viongozi ambao wamechaguliwa na wananchi walio wengi.”
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndugu Maisha Mtipa ambaye amepiga kura katika kituo cha Uwanja wa Ndege Kata ya Sola ambapo baada ya kupiga kura amezungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yameenda vizuri kwa kuwa hakuna malalamiko yoyote yaliyojitokeza na vituo vyote vimefunguliwa saa mbili asubuhi ambapo wananchi tayari wameanza kupiga kura.
Pia akatumia wasaha huo kuwaomba wananchi “nawasihi wananchi wajitokeze waweze kupiga kura waweze kuchagua viongozi wao katika maeneo yao husika”
Pia ameongeza kuwa katika zoezi hilo wananchi wenye mahitaji maalumu wamepewa kipaumbele wanapokuta foleni ambapo wanakwenda moja kwa moja kupiga kura.
Nae Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Mhe. Stanslaus Nyongo amepiga kura katika kituo cha Uwanja wa Ndege Kata ya Sola Wilayani Maswa ambapo amesema katika kituo alichopigia kura hali ya usalama ni shwari na zoezi linaendelea vizuri.
Pia Mhe Nyongo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi hao kwa kuwa muda uliobaki ni mchache.
Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Maswa wamewapongeza wasimamizi wa uchaguzi kwa kuweka utaratibu mzuri wa kupiga kura kwasababu wananchi hao wamesema wametumia muda mchache kupiga kura na kuondoka kuendelea na majukumu yao.
Picha mbalimbali katika matukio ya leo
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.