Leo tarehe 20/3/2019 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa amekabidhi Zahanati mbili kwa mdau wa maendeleo ( World Vision) ambazo zilikuwa hazijakamilika ili azifanyie ukamilishaji. Mdau huyu ameamua kuunga juhudi za Wananchi kwa kukamilisha majengo mawili ya Zahanati katika vijiji vya Mwatumbe na Wigelekelo Wilayani hapa.
Katika makabidhiano hayo mdau huyu wa maendeleo amemkabidhi pia Mkandarasi mteule Ms. Kalumo Technology Investement Limited kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo kwa mujibu wa BOQ iliyoandaliwa kufanya ukamilishaji. Mkataba uliofungwa kati ya World Vision na Mkandarasi kazi ilitakiwa kuanza tarehe 11/3/2019 na kukamilika tarehe 31/5/2019. Pamoja na mdau huyu kuunga mkono kazi ya Wanajamii, wananchi wamekumbushwa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kuweza kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ikiwa ni pamoja na kukamilisha majukumu yanayowahusu katika eneo la kazi.
Wananchi wa vijiji vyote wamekumbushwa kuwa ili zahanati kufunguliwa na kuanza kazi vifuatavyo viwe vimekamilika; Jengo la Zahanati, Nyumba ya Mtumishi, Choo, Sehemu ya kuchomea taka ngumu na kutupia Kondo la nyuma. Wananchi wamekubaliana na kuahidi kutoa ushirikiano na kutekeleza wanayotakiwa kukamilisha.
Kutokana na utayari wa wananchi kujitolea kukamilisha majukumu yaliyoonekana kuwa mengi, Waratibu wa Mradi kutoka katika ADP ya Isanga na Shishiyu wameahidi kuendelea kuongeza nguvu ya kuwaunga mkono wananchi. Kwa kuunga mkono muitikio wa Wananchi Mratibu wa ADP ya Shishiyu alisema, " Kutokana na mahitaji kuwa mengi ili kituo kiwe tayari kutumika, tuko tayari kushirikiana nanyi kujenga choo"
Baada ya makabidhiano hayo na mkandarasi kesho kazi inaanza rasmi.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.