Akina mama Ipililo wapata elimu ya namna ya kutumia mlo kamili kwa ajili ya watoto wa miaka 0-5 kwa kufundishwa namna ya kupika uji uliozingatia makundi matano ya vyakula.
“Lishe iliyobora ndio afya ya binadamu tunazungumzia lishe kwa watoto kwa sababu akili inatengenezwa wakati wa utoto usije ukasema mtoto wa mtu fulani ana akili nzuri au anafanya vizuri darasani kwa sababu ya lishe bora, sio bora lishe”
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mpollo Adorat aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya katika kilele cha wiki ya unyonyeshaji duniani pamoja na siku ya afya na lishe ambayo imefanyika leo tarehe 1 machi 2023 katika viwanja vya Kituo cha Afya Ipililo kilichopo Kijiji cha Ipililo Kata ya Ipililo.
Dkt Adorat amesema katika Mkoa wa Simiyu udumavu upo kwa asilimia 33% hivyo serikali chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imempa dhamana Mkuu wa Wilaya kusimamia suala zima la afya ili kuondoa udumavu nchini Tanzania ili watoto wote kuanzia miaka 0-5 wawe safi.
Aidha, Mganga Mkuu amewasisitiza akina mama kuwa jukumu la kulisha watoto ni la kwao hivyo akina mama hao wanatakiwa kuwapa watoto wao mlo kamili ambao unahusisha makundi yote ya vyakula kwa sababu Maswa ina nyakula vya kutosha ambavyo vitamsaidia mtoto kuwa na afya bora ili kuepuka utapiamlo unaosababisha udumavu.
Kwa upande wake Afisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Gyunda ametoa elimu kwa akina mama hao ya namna ya kutumia mlo kamili kwa ajili ya kuwapa watoto wao kwa kuzingatia makundi matano ya vyakula ambayo ni vyakula vya nafaka, ndizi na mizizi, vyakula vya jamii ya mikunde na nyama, mbogamboga zote, matunda pamoja na sukari, mafuta, asali na chumvi.
Pia Afisa Lishe amesema makundi hayo matano ya vyakula yatamsaidia mtoto na mama mjamzito kuwa na nguvu, kuongeza kinga mwilini na kutoa vitamini, kuimarisha mwili pamoja na kuupatia mwili nishati ili kuepukana na kupata maradhi mbalimbali.
Ameendelea kusisitiza kuwa maziwa ya mama ya mwanzo ndio chanjo ya kwanza ya mtoto kwa kuwa yana mlo kamili ambao unajumuisha makundi yote ya vyakula ambavyo ni wanga, protini, madini, vitamini vitakavyomsaidia mtoto kuwa na akili na afya nzuri ili kuepukana na maradhi mbalimbali.
Diwani wa Kata ya Ipililo Mhe: Sayi Samwel Maige amewashukuru viongozi wote wa Wilaya ya Maswa kwa kupeleka Elimu hiyo ya lishe bora katika kata yake na amewaomba akina mama wote kusikiliza kwa makini Elimu hiyo ili ikawasaidie watoto wao.
Nae Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mwagala Ndg. James Hongoli amesema maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ni kuhakikisha watoto, akina mama na wananchi wote katika kila Kijiji na Kata wanapata Elimu ili iwasaidie katika kuboresha afya za familia zao.
"Serikali kwa ujumla wake inaamini kabisa wananchi wanazalisha vyakula mbalimbali iIa sasa namna ya kuviandaa vile vyakula kutengeneza mlo kamili hapo ndio pana shida” amesema Hongoli.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.