Wananchi wa Kata ya Jija wamejitokeza kushiriki zoezi la upandaji miti katika chanzo cha Maji kilichoko katika kijiji cha Jija leo siku ya maadhimisho ya sherehe ya wiki ya maji iliyoadhimishwa katika eneo la viwanja vya mnada kijijini hapo. Lengo la upandaji miti katika eneo hilo ni ishara ya kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji. Zoezi la upandaji miti limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Dk. Seif Shekalage ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Zoezi hilo limeambatana na ukaguzi wa mradi wa maji Jija ambao bado uko kwenye matazamio baada ya ukamilishaji. Mradi huu umegharimu Tsh. 249,450,000/= hadi kukamilika na umetekelezwa na mkandarasi aitwaye MMETO wa DSM. Ujenzi wa mradi huu umehusisha ujenzi wa tanki la lita 50,000, ujenzi wa vituo 13 vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba ya mtambo, ujenzi wa kituo cha kunyweshea mifugo na ufungaji wa pampu ya kusukuma maji. Maadhimisho ya Wiki ya maji kwa mwaka 2018 kitaifa yalikuwa na kauli mbiu isemayo "HIFADHI MAJI NA MFUMO WA KIIKOLOJIA KWA MAENDELEO YA JAMII".
Kupitia maadhimisho haya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe. Lucas Hinda Mwaniyuki ameipongeza idara ya maji kwa jitihada wanazozifanya ili kutekeleza zoezi zima la kufikisha huduma ya maji katika jamii ( vijiji vya Maswa) na ameomba waendelee kujitahidi hivyo ili kila kijiji chenye shida ya maji kiweze kupata huduma hiyo mhimu.
Pia Mgeni rasmi amewataka wananchi kutunza mazingira yanayozunguka maeneo ya vyanzo vya maji. Amaetumia muda huo kuihasa Kamati ya maji kusimamia kikamilifu na kukagua vema vituo vyote vya kuchotea maji ili kubaini changamoto zilizopo kabla ya kukabidhiwa mradi na Mkandarasi.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.