Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amewataka wananchi wa Maswa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kupata vitambulisho ambavyo vitawawezesha wananchi hao kupata haki yao ya msingi ya kikatiba ya kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka .
Pia ameongeza kuwa zoezi hilo litawahusu wananchi wote ambao wamefikisha umri wa miaka 18, waliopoteza vitambulisho pamoja na wananchi waliohama eneo walilojiandikisha wakati wa kupiga kura mwaka 2020.
Mkuu wa Wilaya amesema hayo wakati wa ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji Cha Shinyangamwenge Kilichopo Kata ya Dakama tarehe 17 Julai 2024.
"Wale ambao walikuwa hawajafikisha miaka 18 sasa ni wakati wao wa kwenda kujiandikisha ili wawemo katika daftari la kudumu la wapiga kura ili mwaka 2025 wakaweze kupiga kura lakini pia ni kwa wale ambao wamehamia kutoka sehemu nyingine,
mfano wametoka Mpanda Katavi na Rukwa wamehamia Shinyangamwenge sasa ili uweze kupiga kura unatakiwa ujiandikishe hapa na taarifa zako wakati wa kupiga kura zitakuwa hapa." Mhe Kaminyoge
Pia Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa wananchi ambao wataboresha taarifa zao pindi zoezi hilo litakapotangazwa kuanza kuhakikisha wanakwenda na vitambulisho hivyo vya mpiga kura ili taarifa hizo ziweze kuboreshwa.
Katika hatua nyingine Mhe Kaminyoge amewaomba wananchi kuwalinda watoto wenye ulemavu wa ngozi ili wasipate madhara kutokana na mila potofu zinazofanywa na wagaga wa kienyeji ambao hawana vibali kutoka ofisi ya Mkurugenzi kupitia kwa mganga Mkuu wa Wilaya ambao wanatumia lamli chonganishi.
"Wale waganga wa kienyeji ni wale waganga ambao hawana vibali wanapiga lamli chonganishi mtu anakwenda anasema ili uwe tajiri unatakiwa ufanye moja mbili tatu na mtu akisikia utajiri anaondoka anaenda kutekeleza la kutekeleza anadhuru miasha ya mtu, utajili asipate, mtu anakufa, wananchi tunaomba walindeni albino kwa nafasi zenu." Amesema Mkuu wa Wilaya
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya amesikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi zikiwemo za afya, maji, vitamburisho vya NIDA pamoja na elimu.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.